KAMATI iliyokuwa ikichunguza vurugu zilizotokea
mkoani Iringa na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mwandishi wa Kituo Cha
Televisheni cha Channel Ten, David Mwangosi imekabidhi ripoti yake kwa
Waziri wa Mambo ya Ndani Dk Emaanuel Nchimbi.
Katika vurugu hizo
ambazo zilizotokea Kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi Septemba 2 mwaka
huu, kati ya Polisi na wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi la
Chama hicho baadhi ya watu walijeruhiwa akiwemo askari wa jeshi hilo.
Taarifa
iliyotolewa jana na Msemaji wa Wizara hiyo Isaac Nantanga ilisema
kamati hiyo imekamilisha kazi iliyopewa na hivyo kusubibili kikao cha
kamati hiyo na waziri wiki ijayo.
“Waziri ameishukuru kamati hiyo
kwa kazi walioifanya na Jumanne (kesho kutwa) atafanya kikao na
waandishi wa habari” alisema Nantanga.
Wakati akiitangaza kamati hiyo Dk Nchimbi aliitaka kujibu maswali sita ambayo yalikuwa hanaya majibu kutokana na tukio hilo.
“Tuna
maswali sita ambayo mimi sina majibu yake. Swali la kwanza tunataka
kujua nini chanzo cha kifo cha Daudi? Pili tujue ni kweli kwamba kuna
uhasama kati ya polisi na waandishi Iringa?” alisema Dk Nchimbi
Aliongeza:
“Tatu tujue kama ni kweli kuna orodha ya waandishi watatu wa
kushughulikiwa Iringa? Nne kama nguvu zilizotumika zilistahili? Tano
kama kuna utaratibu wa vyama vya siasa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa
polisi? Mwisho kujua uhusiano wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa
ukoje?”
Dk Nchimbi alisema, sheria lazima zifuatwe kwani nchi
ikiingia kwenye matatizo, Serikali haitaweza kuwaeleza wananchi kwamba
ndicho kitu kinachotakiwa... “Hatutaki tuwe na vita vya wenyewe kwa
wenyewe.”
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Theophil Makunga alisema kamati yake ilifanya ziara katika mikoa ya
Iringa na Dar es Salaam na kufanya mahojiano na wadau mbalimbali.
Alisema
wakati wa zoezi hilo walizingatia yale waliyoelezwa na Dk Nchimbi ikiwa
ni kufanya kazi kwa kuweka mbele maslahi ya taifa.
“Alitutaka
kufanya kazi bila kuegemea upande mmoja wa Serikali ama chama na
tumejibu maswali yote yaliyokuwa katika habibu za rejea alizotupa bila
kuacha hata moja,” alisema Makunga.
Aliongeza licha ya kujibu habibu hizo za rejea pia tumetoa mapendekezo ambayo kama yatatekelezwa hakutatokea tukio kama hilo.
Alipotakiwa
kueleza kilichomo ndani ya ripoti hiyo alisema hawezi na kutaka
kusubiri Jumanne ambapo Waziri na Kamati nzima itazungumza na waandishi
wa habari.
Kamati hiyo ilikuwa watu watano ambayo ilikukuwa
chini ya Mwenyekiti , Jaji mstaafu Steven Ihema, mwakilishi wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga,
Wajumbe wengine
walikuwa ni mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili
Mtambalike, mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishina wa Polisi (DCP), Isaya
Mngulu.
0 Comments