MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji
(Ewura) imetoa bei kikomo mpya ambazo zitaanza kutumika leo nchini kote
ikiwa imeshuka kwa Sh 306, kwa lita ya petroli, Sh 192 kwa lita moja ya
dizeli huku mafuta ya taa bei ikibaki bila kubadilika.
Taarifa
iliyotolewa jana na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus
Kaguo, ilisema bei za mafuta ya petroli kwa Dar es Salaam itakuwa Sh
1,994 kwa lita moja ikiwa imeshuka kutoka Sh2,300 ya bei ya Septemba.
Alisema mafuta ya dizeli bei yake imeshuka hadi kufikia Sh1,950 kutoka
Sh2,142, wakati mafuta ya taa yanabakia Sh1,993 kutokana na kutoingia
meli yoyote ya mafuta hayo.
Taarifa hiyo ilisema bei hizo,
zitaendelea kuongezeka kutokana na gharama za usafirishaji kutoka Dar es
Salaam kwenda mikoani, ingawa kwa ujumla katika kila eneo punguzo
litakuwa ni Sh 306 na Sh 192 kwa petroli na dizeli kwa kila lita moja.
“Kwa
mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya
petroli zitaendelea kupangwa na soko na Ewura itaendelea kuhamasisha
ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta,”alisema
na kuongeza; “Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya
uamuzi stahiki kuhusu ununuzi wa bidhaa za mafuta kulingana na bei
anayoiona mteja inamfaa.” Kaguo alisema kampuni za mafuta zipo huru
kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo
ziwe chini ya bei kikomo na kama mfanyabiashara atakiuka atapewa adhabu
ya kulipa Sh3 milioni. Pia alivitaka vituo vyote vya mafuta
kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana
ili mteja afanye uchaguzi wa kununua mafuta akiwa anajua bei halisi ya
mafuta katika kituo husika.
“Wanunuzi wanashauriwa kuhakikisha
kuwa wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe,
aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita kwani stakabadhi hiyo ya
malipo itatumika kama kidhibiti cha ununuzi wa mafuta endapo
kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei
kikomo; ama endapo utakuwa umeuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora
kisichofaa,” aliongeza Kaguo.
Hivi karibuni Baraza la Ushindani
wa Haki (FCC), lilitupilia mbali rufani ya kampuni 13
zinazojishughulisha na uuzaji wa mafuta, zilizokuwa zinapinga kanuni
mpya ya kukokotoa bei za mafuta iliyobuniwa na Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (Ewura). Katika hukumu hiyo iliyotolewa wiki iliyopita,
Mwenyekiti wa baraza hilo, Razia Sheikh, alisema uamuzi wa kuitupa
rufani hiyo ulitokana na warufani, kushindwa kuthibitisha madai yao
kikamilifu.
Alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote
mbili, baraza liliridhika kuwa Ewura ilikuwa imefuata taratibu zote
zilizowekwa kisheria, kabla ya kutangaza kanuni mpya za kukokotoa bei za
mafuta nchini. Katika usikilizaji wa shauri hilo, Mwenyekiti Sheikh
alisaidiwa na wajumbe wawili ambao ni Malima Bundala na Ali Juma.
Kampuni
zilizokata rufaa ya kupinga uamuzi wa Ewura ni pamoja na BP Tanzania
Limited, Engen Petroleum Tanzania Limited, Camel Oil Tanzania Limited,
Oilcom Tanzania Limited, Total Tanzania Limited, Gapco Tanzania Limited
na Hass Petroleum Tanzania Limited. Nyingine ni Orxy Oil Company
Limited, MSG International Tanzania Limites, GBP Tanzania Limited, Lake
Oil Limited, Moil Tanzania Limited and Acer Petroleum Tanzania Limited.
Pamoja na kutupilia mbali rufani hiyo, Sheikh pia aliziamuru
kampuni hizo kulipa gharama za kesi. Kwa mujibu nyaraka za baraza
hilo, gharama za mawakili wa Ewura peke yake ni zaidi ya Sh100 milioni.
Pamoja na mambo mengine, kampuni hizo zililiomba baraza hilo kuifuta
kanuni hiyo mpya kwa vigezo kuwa, Ewura haikufikiria mambo kadhaa kabla
ya kuitangaza.
0 Comments