Watu wawili wamefariki dunia papo
hapo, akiwamo askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
Koplo William Mwaikambo, na wengine sita kujeruhiwa kufuatia gari la
jeshi hilo kugongana uso kwa uso na gari la kiraia aina ya Toyota
Coaster.
Koplo Mwaikambo alikuwa ni dereva wa gari la Makao Makuu ya JWTZ.
Tukio hilo lilitokea jana jijini Dar es Salaam, eneo la Kwa Warioba,
Mikocheni, wakati gari la jeshi likitokea makao makuu ya jeshi
likirudisha walinzi Lugalo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na makao makuu ya JWTZ
ilieleza kuwa daladala lililokuwa likiendeshwa na Musa Hamad Rajabu
lililipita gari aina ya DCM na kuhamia upande wa pili wa barabara na
kisha kugongana uso kwa uso na gari la jeshi.
Taarifa hiyo imewataja waliojeruhiwa kuwa ni Luteni Kileo, Praveti
Charles Mwamnyanyi, Praveti Godbless Manyanga, Koplo Fred Nkamata na
Praveti Shimoti Nicademus, wote wa JWTZ, pamoja na raia, Mohamed Omari.
Wote wamelazwa katika Hospitali ya Lugalo na taratibu za mazishi ya askari aliyefariki zinaandaliwa.
0 Comments