
Polisi Kenya wakidhibiti moja ya eneo lililoshambuliwa
TAKRIBANI askari 10 wa Jeshi la Polisi Kenya
wamejeruhiwa vibaya katika shambulizi la guruneti. Maofisa hao wa polisi
walikuwa wakiendesha msako katika nyumba moja mjini Mombasa, pwani mwa
Kenya, ambako walifanikiwa kukamata silaha ikiwemo bunduki aina ya AK-47
na maguruneti mawili.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Kenya anasema kuwa huwenda wanamgambo wa Al-Shabab wamehusika na shambulizi hilo.
Kenya kwa muda sasa imakumbwa na mfululizo wa mashambulizi ya
maguruneti, tangu wanajeshi wake walipoingia nchini Somalia kupambana na
wanamgambo wa Al Shabaab mwaka jana.
Mkuu wa Polisi mkoani humo, Aggrey Adoli, amewaeleza waandishi wa
habari watu watatu wanaoshukiwa kufanya shambulio hilo la kigaidi
waliuawa katika makabaliano kati yao na polisi baada ya shambulizi hilo.
Washukiwa wa Al-Shabab wametekeleza mashambulizi kadhaa katika kipindi
cha mwaka mmoja uliopita eneo la Pwani ambalo ni maarufu kwa watalii.
Wanajeshi wa Kenya nao wamekuwa vitani kuondoa kundi la Al Shabaab
kutoka katika ngome yao kubwa na ya mwisho ambayo ni Kismayo kwa
ushirikiano na wanajeshi wa Muungano wa Afrika tangu Oktoba mwaka jana,
jambo ambalo walifanikisha mwanzoni mwa mwezi huu.
-BBC
0 Comments