Ajali ya Hiace yaua watano, yajeruhi 14

Ajali ya Gari Hiace

 Na Sharon Sauwa

Watu watano wamefariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T 803 ABX kuacha njia na kupinduka wilayani Bahi mkoni hapa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa, ajali hiyo ilitokea jana saa 10:00 jioni katika eneo la Bahi Relini.

Mkwasa alisema Hiace hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Yohana Samson, ilikuwa ikitokea Dodoma kwenda katika eneo la Makanda.

Alisema Hiace hiyo iliacha njia baada ya lori aina ya Scania lilokuwa likiendeshwa na Tutu Jackson kutaka kuipita Hiace hiyo, lakini ghafla liliigonga kwa nyuma na ilipinduka.

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Stephen Zelothe, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuahidi kutoa taarifa leo.

“Ajali ipo, lakini ninatoa taarifa kesho (leo),” alisema kwa kifupi Zelothe.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodom, Zainabu Chaula, alipotafutwa alijibu: "Mimi niko wodini huku nawaangalia wagonjwa"

Habari zaidi kutoka katika eneo hilo zilisema miili ya watu watatu ilitambuliwa na ndugu zao jana jioni.

Post a Comment

0 Comments