Waandishi wamtimua Waziri Dk Nchimbi


*NI BAADA YA KUVAMIA MAANDAMANO YAO,WENZAO IRINGA WAANGUA VILIO MKUTANONI

Waandishi Wetu

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi jana alionja shubiri ya hasira za waandishi wa habari, baada ya kutimuliwa kwenye maandamano yao waliyoyafanya Dar es Salaam kulaani mauaji ya mwenzao Daudi Mwangosi.

Maandamano hayo yaliyoanzia katika Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, yamefanyika ikiwa zimepita siku 10 tangu kuuawa kwa Mwangosi ambaye alikuwa mwandishi wa kituo hicho, mkoani Iringa.

Mwangosi aliuawa kwa bomu la machozi wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa Chadema waliokuwa katika sherehe za kuzindua tawi lao katika Kijiji cha Nyololo, Iringa, Septemba 2, mwaka huu.

Dk Nchimbi alifukuzwa na kuzomewa muda mfupi baada ya maandamano hayo kufika katika Viwanja vya Jangwani ambako yalihitimishwa kwa matamko mbalimbali.

Waziri huyo alifika kwenye viwanja hivyo sambamba na maandamano hayo na kusimama pembeni karibu na eneo ambalo waandishi walikuwa wakikusanyika.

Baada ya viongozi wa maandamano hayo kupita kuelekea mbele, Dk Nchimbi aliungana nao jambo lililopokewa kwa hisia tofauti na idadi kubwa ya wanahabari hao ambao walianza kuhoji ujio wake, lakini kikubwa wakitaka aondolewe.

“Umekuja kufanya nini, kwani sisi tulikualika?” alisikika akisema mmoja wa waandishi hao.
Baada ya swali hilo, Waziri Nchimbi aliomba apewe risala iliyoandaliwa na waandishi hao, lakini kinyume chake alijibiwa kuwa risala ni mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kulaani mauaji hayo, hivyo na kumtaka ayasome kwa umakini.

Baadhi ya mabango hayo yalisomeka: “Tunaomba mamlaka kuunda tume huru ya uchunguzi wa mauaji ya Daudi Mwangosi.... Tunasikitika na tunalaani mauaji ya mwandishi wetu mkoani Iringa.”

Mabango mengine yalisomeka: “Mwema (IGP) unangoja nini?, Kalamu na kamera zetu ni zaidi ya risasi na mabomu yao, polisi wawajibike, damu ya Mwangosi isafishe Jeshi la Polisi.

Mengine yaliyosomeka: “Polisi wamemuua Mwangosi,Hatunyamazi kwa mtutu wa bunduki.... Mtatuua lakini tutaandika ukweli, Why killing the messenger? [Kwa nini mnamuua mjumbe?] na polisi kutuua basi.

Wakati waandishi wakipiga kelele kutaka waziri huyo aondoke, aliendelea kuwapo eneo hilo, huku akitabasamu na kujaribu kuomba kuzungumza.

Kitendo hicho kiliwafanya waandishi kuanza kumzomea, huku wakimtaka aondoke eneo hilo kwa kuwa hakualikwa na maandamano hayo yalipaswa kuhutubiwa na waandishi wenyewe kupitia kwa viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Huku akiwa haamini kinachoendelea na mzozo huo kutimia dakika saba, mwandishi wa habari mwandamizi, Nyaronyo Kicheere alikwenda kupaza sauti akimwambia kinagaubaga waziri huyo kwamba mkutano huo haumhusu wala kiongozi yeyote wa Serikali.

“Haya ni maandamano ya waandishi wa habari, hatukumwalika kiongozi yeyote wa siasa au Serikali,” alisema Nyaronyo huku akishangiliwa na waandishi wenzake.

Mbali na kupiga kelele za kumtaka Waziri Nchimbi aondoke, waandishi hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za mshikamano, sambamba na kuonyesha picha za marehemu Mwangosi.

Mwishowe, Waziri Nchimbi aliyekuwa amevalia kaunda suti ya rangi ya maziwa, aliamua kuondoka kwa unyonge, huku akisindikizwa kwa kelele za kumzomea.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuondolewa eneo hilo, Waziri Nchimbi alisema Serikali inawathamini waandishi wa habari na itaendelea kushirikiana nao.

“Kupitia fursa hii naomba niwaagize makamanda wa polisi wa mikoa kuandaa mikutano na waandishi wa habari ili kujenga mazingira mazuri ya kufanya kazi, kwa maana hatuwezi kuendelea katika hali kama hii,” alisema Waziri Nchimbi.

Matukio mengine
Maandamano hayo pia yaliambatana na matukio mengine kadhaa ikiwamo waandishi kulala barabarani, huku wengine wakiigiza kuua kwa mtutu wa bunduki.

Uliibuka pia mjadala wa wanahabari hao kutumia moja ya magari yaliyokuwa yakisindikiza maandamano hayo kama jukwaa. Hoja hiyo ilipingwa na wazungumzaji wote kulazimika kutumia kifusi cha mchanga uliokusanywa katika eneo hilo.

Waandishi zaidi ya 100 walikutana katika Kituo cha Channel Ten katikati ya jiji la Dar es Salaam na kuanza maandamano  hayo saa 2:48 asubuhi. Walifika Jangwani saa 3:30.

Mbali na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, maandamano hayo pia yaliwashirikisha wanafunzi wa vyuo vya uandishi wa habari kikiwamo cha Dar es Salaam, (DSJ) ambao nao walikuwa na bango lenye ujumbe wa kulaani mauaji hayo.

Vilio, Simanzi vyatawala Iringa
Vilio na simanzi jana vilitawala viunga vya bustani ya Manispaa ya Iringa ambako waandishi wa habari walihitimishia maandamano yao ya amani yaliyoandaliwa kulaani kuuawa kwa mwenzao, Mwangosi.

Machi 6, mwaka huu marehemu Mwangosi alisimama katika bustani hiyo na kutoa tamko la waandishi wa habari kupinga manyanyaso, ubaguzi na vitisho kwao kutoka baadhi ya taasisi za Serikali ikiwamo polisi.

Maandamano hayo yaliyovuta hisia za wadau wa kada mbalimbali wakiwamo wanaharakati wa haki za binadamu, yalianzia katika Ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC) saa 4:15 asubuhi.

Karibu muda wote wa maandamano hayo, waandishi hao walikuwa wakilia kiasi cha kuwafanya hata baadhi ya wananchi waliowashuhudia wakipita katika mitaa kadhaa ya Manispaa ya Iringa nao kububujikwa na machozi.

Mratibu wa maandamano hayo, Zulfa Shomari alisema hicho ni kielelezo na ishara ya kulaani ukatili uliofanywa dhidi ya mwandishi huyo akiwa anatekeleza majukumu yake.

“Sisi wanahabari Mkoa wa Iringa tunaungana na wenzetu nchini kulaani vikali mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya Mwangosi ambaye alikuwa akitekeleza wajibu wake wakati Chadema wakiendesha shughuli zao za ndani za kichama,” alisema Shomari.

Alisema licha ya tukio hilo, wataendelea na msimamo wao wa kutoshirikiana na polisi mpaka kamati iliyoundwa itakapotoa taarifa zenye ukweli na kuridhisha kuhusu mauaji hayo ikiwa ni pamoja na watuhumiwa kufikishwa mahakamani.

“Nashangaa kuona Serikali inapoteza kodi za wananchi kuchunguza mauaji yaliyofanywa na polisi wakati suala liko wazi ikiwamo ushahidi wa picha zilizopigwa wakati mauaji hayo yakitekelezwa,” alisema.

Katibu wa kamati ya maandamano hayo, Daniel Mbega alisema anashangaa kuona Jeshi la Polisi linawashambulia wanahabari wakati wanasaidia kufichua mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma.

“Ninashangaa sana kuona polisi wanaua raia wasiokuwa na hatia kwa kutumia silaha badala ya kuwalinda, utafikiri nchi yetu iko katika vita ya wenyewe kwa wenyewe! Tunachohitaji kufahamu kamera na Laptop ya Mwangosi viko wapi ?” alihoji Mbega.

Imeandikwa na Fidelis Butahe, Aidan Mhando, Ibrahim Yamola, Geofrey Nyang’oro Dar; Frederick Siwale na Clement Sanga, Iringa

Post a Comment

0 Comments