MAANDAMANO ya Waandishi wa habari kulaani mauaji ya Mwandishi
wa habari, Daud Mwangosi yameingia utata baada ya waandishi kumfukuza
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi lakini wakamkaribisha
kada wa CHADEMA kuwahutubia. Utata huo ulijitokeza kwenye viwanja vya
Jangwani, jijini Dar es Salaam, baada ya waandamaniji kufika wakiwa na
viongozi wao wakiwemo kutoka Jukwaa la Wahariri.
Mara msafara huo ulipofika, pembezoni mwa viwanja hivyo, ukakumbana
na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchini alikiwa eneo hilo na
mara akaungana na baadhi ya viongozi wa waandishi, ambao walijaribu
kutaka kumtamtambulisha.
“Hatuatakiii, aondoke, aondoke!” waandishi wa habari kwenye
maandamano hayo walipaza sauti huku wengine wakirusha mikono kuashiria
kukataa kabisa waziri Nchini asizungumze lolote au kuwepo kwenye mkutano
mwishoni mwa maandamano hayo.
Baadhi ya viongozi wa Jukwaa la Wahariri akiwemo Nevilli Meena,
walijaribu kuwatuliza waandishi lakini, ikashindikana na kwa busara
Waziri Nchini akaamua kuondoka. Hata hivyo katika kinachoonesha kwamba
kulikuwepo tofauti kati ya waandishi kuhusu kumkataa Dk. Nchini, baadhi
yao walimfuata na kumhoji, lakini wengine wakaingilia kati kuzuia
mahojiano hayo.
“Sasa tumesema aondoke halafu mnamhoji, mnamhoji nini na tumekataa
hapa asiseme nini? mwacheni njooni kwenye mkutano wetu hapa, kwanza
sijui habari hizo mtazirusha wapi, sisi ndiyo wahariri”, zilisikika
sauti zikipazwa.
Baada ya kuzungumza viongozi mmoja baada ya mwingine, wote wakilaani
kwa nguvu zote mauaji ya Mwangosi, nayoaminika kufanywa na polisi wakati
wa maandamano ya Chadema, Septemba 2, mwaka huu, mkoani Iringa, ndipo
akapandishwa jukwaani Kada wa Chadema, Dk. Azaveri Rweitama. Dk.
Rweitama ambaye amewahi kushiriki shughuli nyingi za Chadema ikiwemo
mikutano ya chama hicho, alipandishwa jukwaani mmoja wa viongozi wa
Jukwaa la Wahariri.
“Jamani mnajua waandishi wa habari tuna marafiki. Sasa hapa tunaye
Dk. Rweitama amabaye ni rafiki yetu atazungumza machache”, alisema
Misango akimkaribisha Dk. Rweitama.
Akizungumza, Reitama aliwataka waandishi wa habari kutowachukia
polisi wadogo akisema, wao siyo tatizo ila tatizo ni wakubwa zao ambao
alidai wanatumwa na wanasiasa kutekeleza matakwa yao.
“Sasa kama Chadema wanafungua matawi ya chama chao, kwa nini utumie
polisi kuwazuia? si na wewe ukafungue matawi yako?” alisema Dk. Reitama
katika moja hoja zake kwenye mkutano huo.
Kufuatia Dk. Reitama kuzungumza habari za vyama vya siasa hadi kutaja
majina, baadhi ya viongozi na waandishi walianza kulauminiana kuonyesha
kwamba walichofanya nin kosa.
“Sisi tulikuwa tumeshakubaliana kwamba asishirikishwe kada wa chama
chochote wala wanaharakati, sasa huyu Rweitama nani amemruhusu kupanda
jukwaani?, alihoji mmoja wa viongozi wa Klabu wa Waandishi wa habari wa
Dar es Salaam.
Maandamano ya waandishi hao yalianzia kituo cha Channel Ten, jijini,
saa tatu asubuhi, na kuendelea hadi kwenye viwanja hivyo vya Jangwani,
baada ya kupitia barabara ya Morogoro. Polisi walisindikiza maandamano
hayo baadhi wakiwa nyuma na gari lao na wengine wakitembea kwa miguu,
hadi kwenye viwanja hivyo, ambako halimalizika salama.
0 Comments