USAFIRI wa reli kwa wakazi wa Dar es Salaam
utazinduliwa rasmi Oktoba mwaka huu kama ilivyopangwa, hata kama baadhi
ya miundombinu itakuwa haijakamilika.Akizungumza ofisini kwake jana,
Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Mohamed Mohamed
alisema hadi sasa kila kitu kinakwenda vizuri ingawa wanakabiliwa na
changamoto nyingi.
Mohamed alisema tayari kandarasi zimetolewa kwa
kampuni tofauti kwa ajili ya ujenzi wa vituo na sehemu za kukatia
tiketi, uwekaji kokoto katika reli, vifusi kwa baadhi ya maeneo, alama
za tahadhari katika makutano ya barabara na umeme na vyoo.
“Kuna
kampuni tumezipa kazi na nyingine tutazipatia kandarasi za huduma hizo,
ili kufanikisha utekelezaji mradi huo ambao utahusisha kilomita 197 za
reli,” alisema.
Alisema bajeti imeongezeka kutokana na kuibuka kwa
changamoto ambazo utekelezaji wake unahitaji fedha, huku TRL ikiwataka
waliopo ndani ya mita 15 kutoka ilipo reli, kuondoka ili kupisha
utekelezaji mradi.
“Kuwapo ndani la eneo la hifadhi ya reli ni
kosa kisheria, hivyo waliojenga maeneo hayo wanatakiwa kuhama haraka
iwezekanavyo badala ya kusubiri kuchukuliwa hatua,” alisema Mohamed.
Mohamed
alisema wamewasiliana na manispaa za Ilala na Kinondoni kuhusiana na
wakazi waliopo makutano ya reli na barabara, ambao wanatakiwa kuwa
umbali mita 92 ili ziangalie jinsi ya kuwaondoa kabla ya kuzinduliwa
mradi.
0 Comments