 |
UJENZI: DARAJA KIGAMBONI Daraja la Kigamboni likiendelea kujengwa
katika Bahari ya Hindi, eneo la Kurasini, Dar es Salaam jana. Daraja
hilo linatarajiwa kuwa na njia sita litakapokamilika na hivyo kuwa
daraja kubwa zaidi katika Afrika Mashariki na Kati. Picha na Aron
Msigwa
|
Na George Njogopa
UJENZI wa Daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam, umeanza kwa
kishindo na jana Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alitembelea eneo
hilo na kuwahimiza makandarasi kukamilisha kazi hiyo kwa muda
uliopangwa.
Daraja hilo linalojengwa na Serikali kwa kushirikiana
na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), linatarajiwa kukamilika katika
kipindi cha miaka mitatu huku likigharimu Sh214 bilioni.
Ujenzi
wa daraja hilo unafanywa na Kampuni ya China Railways Construction na
China Major Bridge Engineering Company, zote za nchini China.
Akizungumza
na makandarasi hao, Waziri Magufuli aliwataka waongeze kasi ya ujenzi
na kuahidi kwamba Serikali itatoa ushirikiano wa hali na mali ili
kukamilisha kazi hiyo.
"Nataka niwahakikishie kwamba Serikali
itaendelea kuwa bega kwa bega nanyi. Lakini najua nyie ni wachapa kazi,
mnaweza kufanya kazi usiku na mchana na kufanya ujenzi uchukue miezi 30
badala ya 36 ya sasa," alisema Dk Magufuli.
Waziri Magufuli pia alitumia fursa hiyo kuwaonya wataalamu hao juu ya kile alichokiita kuendesha ujenzi wa kiwango cha chini.
"Hapa
lazima niwe mkweli kwamba Serikali haitasita kuchukua hatua kali, iwapo
ujenzi huu utafanywa katika hali ya kulipua. Tunataka ubora, tena ubora
unaoeleweka," alisisitiza.
Waziri Magufuli ambaye katika ziara
hiyo aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq
alieleza kufurahishwa na kasi ya ujenzi huo na kuwataka wamalize kazi
kwa wakati kwa kuwa Serikali haitaongeza muda.
0 Comments