WAKATI wanasayansi wakiwa wanakaribia kukamilisha
utafiti wa kuwezesha kupata tiba ya Ukimwi, ugonjwa mpya ambao unafanana
kwa karibu kabisa na huo, umeibuka.
Adult-Onsets Immunal Deficiency (AOI) umeripotiwa kuibuka katika nchi za Ulaya na kusambaa kwa kasi duniani.
Kuibuka
kwa ugonjwa huo, kumesababisha hofu mpya katika nchi za Ulaya na Bara
la Asia ambako wagonjwa wengi zaidi wameonekana kuathiriwa na ugonjwa
huo.
Ugonjwa huu umegunduliwa na Dk Sarah Browne wa Taasisi ya
Mzio na Magonjwa ya Kuambukiza ya nchini Marekani (NIAID) ambaye
aliongoza timu ya wanasayansi walioendesha utafiti husika.
Dk
Browne alisema tofauti na Ukimwi, ugonjwa huo hauambukizwi kwa ngono
wala njia ambazo Ukimwi unaenezwa, ila unadhoofisha kinga za mwili kama
ambavyo virusi vya HIV vinafanya.
Dk Browne katika majibu yake
kwa gazeti hili alisema utafiti uliofanywa katika nchi za Taiwan na
Thailand, umebaini kuwa watu wazima wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi
50 ndio waliogundulika na kuathiriwa zaidi na ugonjwa huu.
“Watu
hao hawakuwa na virusi vya Ukimwi na CD4 zao, (chembe hai nyeupe ambazo
huupa mwili kinga ya magonjwa) zilikuwa sawa,” alisema na kuongeza:
“Bado
hatujahakikisha kama ugonjwa huu mpya umewakumba watu wa Bara la
Afrika, ingawa upo uwezekano kuwa wapo wengi wenye ugonjwa huu hasa kesi
nyingi zinazofananishwa na kifua kikuu au Ukimwi,” alisema Dk Browne.
Jambo
jingine linalochagiza utata katika ugonjwa huo mpya ni kuwa dalili zake
ziligundulika kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea.
Dk Browne alisema mtu hazaliwi na maradhi hayo, bali huyapata ukubwani.
Vilevile,
timu ya wanasayansi hao ilieleza kuwa dalili za ugonjwa huo ambazo
zinafanana kwa asilimia kubwa na dalili za Ukimwi hazikuonekana kwa
ndugu wengine wa familia ya mgonjwa jambo ambalo linathibitisha kuwa
ugonjwa huo si wa kurithi.
“Mwili kwa kawaida, unazalisha
kemikali ambazo zinafanya kazi ya kupigana na vimelea vya magonjwa kila
vinapojitokeza, lakini watu wenye maradhi haya, miili yao inazalisha
vimelea ambavyo vinabadilisha mfumo wa mwili wa kupigana na maradhi,”
alisema Dk Browne
Watafiti hao mpaka sasa bado hawajajua sababu za ugonjwa huo na wanaendelea kukuna vichwa ili kubaini kiini chake.
“Bado
hatujajua nini kinasababisha ugonjwa huu, lakini tulichokijua ni kuwa
watu wanaougua maradhi haya hupata maradhi kama yale yanayoambatana na
Ukimwi yaani pneumonia (ugonjwa wa mapafu), TB, au fangasi,” alisema Dk
Browne.
Jarida la Tiba la nchini Uingereza (New England Journal
of Medicine) linasema kuwa ugonjwa huo ulibainika kwa mara ya kwanza
2004 Mashariki mwa Bara la Asia.
Timu hiyo ya wanasayansi ilifanya
utafiti kwa watu 204 ambao hawajaathirika na VVU, utafiti ambao
ulichukua kipindi cha miezi sita.
Watafiti hao walitathmini damu
za watu hao kwa kutumia kemikali ambazo ziliuwezesha mwili kujikinga
na magonjwa, lakini iligundulika kuwa miili ya baadhi yao inazalisha
kemikali ambazo zinazuia mwili kujikinga na maradhi.
“Wakati HIV
inashambulia na kuharibu seli za mwili yaani kinga ya mwili dhidi ya
maradhi, ugonjwa huo mpya hauathiri seli, lakini mwili unashindwa kutoa
‘amri’ ya kupambana na maradhi,” alisema.
Alisema mwili wa
mgonjwa hushindwa kupigana na maradhi hayo mara baada ya kemikali za
kawaida kuzuiwa zisipigane na hapo ndipo mwili huanza kushambuliwa na
fangasi, kifua, homa na maradhi mengine nyemelezi.
“Ni kama kamanda
wa polisi ambaye anashindwa kutoa amri kwa askari wake warushe risasi
kwa maadui. Katika hali hiyo, polisi (ambao ndiyo seli) wataendelea
kusimama wakati maadui wakishambulia,” alisema.
Shirika la Habari
la Marekani (APA) linaelezea kuwapo kwa tukio la hivi karibuni ambapo
mwanamke mwenye umri wa miaka 62, raia wa Vietnam, alibainika kuwa na
ugonjwa huo.
Mwanamke huyo alianza kuugua homa mfululizo na
kifua kikuu ambapo daktari wake alimtibu bila mafanikio, hadi alipopewa
rufaa ya kwenda Taasisi ya Taifa ya Afya (NIH), Marekani na kugundulika
na ugonjwa huo.
Maradhi hayo yamesababisha mwanamke huyo
kupungua uzito kutoka kilo 41 hadi 30 na bado anatibiwa kwa zaidi ya
mwaka katika kituo hicho cha afya.
Jarida la Promed la nchini
Marekani linasema kuwa madaktari katika kituo cha NIH ambapo mwanamke
huyo amelazwa wanaendelea kumpa tiba mbalimbali ikiwamo dawa za saratani
ambazo zinadaiwa kuzuia vimelea vinavyosababisha maradhi mwilini.
Hata hivyo, Dk Browne alisema changamoto kubwa ni kujua nini kinasababisha maradhi hayo.
Kauli za madaktari nchini
Akizungumzia
kuhusu ugonjwa huo mpya, daktari wa patholojia wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Dk Innocent Mosha, alisema hana taarifa yoyote kuhusu ugonjwa
huo mpya, lakini alisema mwili kukosa kinga ni jambo linaloweza kutokea
wakati wowote hasa kwa watu wanaotumia baadhi ya dawa.
“Kwa
mfano mtu anayetumia dawa zenye kitu kiitwacho steroid, zinashusha
kinga, hata mionzi kwa wagonjwa wa saratani, lakini kinachosababisha
zaidi ni HIV,” alisema Dk Mosha.
Alisema kwa vyovyote hakuna
tishio kubwa juu ya ugonjwa huo kwa sababu hauambukizi kutoka kwa mtu
mmoja kwenda kwa mwingine kama ilivyo kwa VVU.
0 Comments