 |
Mbunge
wa Rungwe ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, asiye na Wizara
Maalumu , Profesa Mark Mwandosya akiaga mwili wa marehemu Daudi
Mwangosi akiyezikwa juzi katika Kijiji cha Busoka wilayani Rungwe.
Picha na Hawa Mathias
|
POLISI WALIOTEKELEZA OPERESHENI WADAIWA KUSAFIRISHWA KUTOKA
MIKOA MINGINE, WAANDISHI WA HABARI IRINGA WASUSIA MKUTANO WA DCI MANUMBA
Waandishi wetu, Dar, mikoani
INADAIWA kwamba askari waliokuwa katika
operesheni ya kuzuia mkutano wa Chadema katika eneo la Nyololo wilayani
Mufindi, Iringa na ambayo ilisababisha kifo cha Mwandishi wa Habari,
Daudi Mwangosi walitolewa katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Mbeya.
Tayari
tukio hilo limeibua mjadala mzito kiasi cha kumfanya Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kuunda tume huru kubaini chanzo cha
tukio hilo. Marehemu Mwangosi alizikwa juzi nyumbani kwao Tukuyu, mkoani
Mbeya.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zilisema
kuwa polisi hao kutoka mikoa hiyo mitatu wakiwa wamesheheni vifaa
mbalimbali likiwamo gari la maji ya kuwasha, walisafiri siku moja kabla
ya mkutano huo wa Chadema na baadaye kuzuka vurugu zilizosababisha kifo
hicho.
Marehemu Mwangosi aliuawa kwa mlipuko unaodhaniwa kuwa ni wa bomu ambao ulisambaratisha vibaya sehemu kubwa ya mwili wake.
Chanzo
cha habari kutoka mkoani Dodoma kilisema: “Hapa kwetu kuna askari 10 na
tunawafahamu kwa majina. Waliondoka hapa siku moja kabla ya tukio hilo
wakiwa na gari la washawasha.”
Chanzo hicho kilisema kwamba awali,
hawakuwa wakifahamu kama baadhi ya wenzao walichukuliwa na kupelekwa
Iringa. “Tulikuja kuona kwenye gazeti picha na tulipofuatilia tukaelezwa
kuwa ni kweli Dodoma ilitoa askari kwenda Iringa.”
Askari
mwingine aliyekuwa katika operesheni hiyo ambaye jina lake tunalihifadhi
kwa sababu za kitaaluma, alikiri kuwa hadi jana baadhi yao walikuwa
bado wako Iringa na kwamba walikwenda kwa agizo la wakubwa wake wa kazi.
“Sisi
ni Watanzania, lakini tumelazimika kuyafanya hayo kwa sababu ya mkate
(malipo). Kwa kweli haikuwa haki, kuwatoa askari na silaha kutoka mikoa
mitatu kana kwamba wanakwenda kupigana vita!”
Alidokeza kwamba,
askari wote waliotoka Dodoma walikuwa njiani kurudi mkoani humo, jana
lakini gari la maji ya kuwasha liliendelea kubaki huko Iringa likiwa na
dereva wake na askari mmoja mwenye cheo cha inspekta. Askari huyo
alisema kwamba gari hilo lililazimika kubaki kutokana na hitilafu.
“Wengine
wamerudi lakini, kuna wengine wenye gari la kuwasha bado walikuwa
Iringa, gari lao limepata hitilafu kidogo,” kilisema chanzo hicho kutoka
mjini Dodoma.
Mmoja wa askari hao alidaiwa kwamba hiyo inaweza
kuwa moja ya sababu ya askari hao kumshambulia marehemu Mwangosi wakati
mwenzao anayemfahamu akijaribu kuwazuia. "Hii inaonyesha kuwa askari hao
waliompiga walikuwa hawamjui na huyu aliyekuwa akiwazuia, alimjua.”
Makamanda watupiana mpira
Alipoulizwa
kuhusu taarifa hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen
hakukubali wala kukanusha na badala yake alisema: “Mambo yote hayo
yanatakiwa kujibiwa na Kamanda wa Iringa.”
Aidha, alisema sakata la
kifo cha mwandishi huyo kwa sasa liko katika vyombo vya uchunguzi hivyo
asingekuwa tayari kulizungumzia.
“Siwezi kusema kama askari wangu
walikwenda huko au hawakwenda, isipokuwa ninachoweza kusema ni kwamba
suala hilo lipo katika vyombo husika hivyo waachiwe wao au Kamanda wa
Iringa ndiye mwenye majibu.”
Alipotajiwa jina la mmoja wa askari
aliyeonekana katika picha za video na magazeti za tukio hilo kwamba
anatokea katika moja ya vituo vyake, kamanda huyo alisema: “Mimi
yakitokea Dodoma nitazungumza wala siyo mtu mwingine kwa hiyo, mambo ya
Iringa siwezi kuyazungumza na kama tutaanza kila Kamanda kuzungumza
jambo hilo hamuoni kuwa itakuwa ni kama vurugu?”
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alipopigiwa simu yake iliita tu bila kupokewa.
Kwa
upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile
alisema kwa kuwa tukio hilo limefanywa na polisi, mambo mengi
yatazungumzwa lakini akasisitiza kwamba hajapeleka askari Iringa.
Alisema
hakukuwa na agizo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi wala ombi
kutoka Polisi Iringa kutaka askari wa kuongeza nguvu... “Taarifa hizo ni
za uzushi kwani hazina ukweli wowote.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mbeya, Athuman Diwani alikanusha pia kuwapeleka askari wake Iringa
akisema: “Hizo taarifa siyo za kweli. Hakuna askari yeyote aliyekwenda
Iringa wakati wa vurugu zile.”
Mkutano wa DCI wavunjika
Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba hakutaka
kuzungumzia suala hilo akisema: “Hayo yote yameundiwa tume ngoja
tuiachie ifanye kazi yake.”
Awali, DCI Manumba aliitisha mkutano na
waandishi wa habari mkoani Iringa, ambao hata hivyo, ulivunjika baada ya
kutokea kutoelewana baina yao.
Manumba alitaka kueleza ripoti ya
uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, lakini waandishi hao walikataa
kumsikiliza wakisema hawauamini uchunguzi huo kwa kuwa ulifanywa na
polisi peke yao.
Kabla Manumba, hajaanza kuzungumza, Katibu wa
Chama cha Waandishi wa Habari Iringa (IPC), Frank Leonard alisema
kutokana na msimamo wa waandishi wa habari wa mkoa huo hakutakuwa na
uhusiano wa kikazi na polisi hadi pale tume zilizoundwa kuchunguza kifo
hicho zitakapotoa taarifa sahihi juu ya mauaji hayo.
“Msimamo
wetu ni kusitisha uhusiano wa kikazi baina yetu na jeshi la polisi
hususan Mkoa wa Iringa, tumekuja hapa kwa sababu DCI umetuita na kama
unataka kutupa taarifa ya kifo cha ndugu yetu basi waambie hao maofisa
wa jeshi wa Iringa watoke nje,” alisema Leonard.
Akijibu madai
hayo Manumba alisema: “Nia yangu ni kutoa taarifa ya uchunguzi wa kifo
cha Mwangosi, ndiyo maana niliwasiliana na mwenzenu ili tuweze
kuzungumza, Polisi Iringa wataendelea kuwepo na waandishi wa habari
mtaendelea kuwepo, matukio kama haya yapo na yataendelea kuwepo.”
Licha ya maelezo hayo, hakuna mwafaka uliofikiwa na mkutano huo ukavunjika.
Akizungumza
kwa simu na gazeti hili baadaye, DCI Manumba alisema: "Ni vyema wao
wangenisikiliza kujua ninataka kuwaambia nini. Lakini, kwa kuwa kuna
mkanganyiko, nimeona ni vyema jambo hili lisubiri tume ndipo watakuja
kulizungumza.”
Waikataa Tume ya Nchimbi
Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) kimeiponda tume ya Dk Nchimbi kikieleza kuwa
imeundwa ili kurudisha uhusiano kati ya Polisi na waandishi wa habari na
si kutafuta chanzo cha tatizo.
Juzi, Dk Nchimbi alitangaza
kamati ya kuchunguza mauaji hayo inayoongozwa na Jaji Mstaafu, Steven
Ihema na wajumbe, Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Theophil Makunga, Mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili
Mtambalike, Mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya
Mngulu.
Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa
Chadema, Tundu Lissu alisema Dar es Salaam jana kwamba: “Hii si tume ya
kuchunguza mauaji, bali ina lengo la kurudisha uhusiano mzuri kati ya
Jeshi la Polisi na waandishi wa habari ili kuwasahaulisha wananchi kwa
sababu imeundwa na waziri ambaye naye anatakiwa kuhojiwa.” “Tunamwomba
Rais Jakaya Kikwete ateue tume kama anavyoelekezwa na Sheria ya Tume za
Uchunguzi ya mwaka 1992, ambayo inaruhusu kumhoji yeyote kasoro yeye
Rais.”
Lissu alisema Rais Kikwete angeunda tume hiyo na Waziri
Nchimbi na IGP Said Mwema wanatakiwa kujiuzulu ili kupisha uchunguzi
akidai kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba walitoa amri ya mauaji hayo.
“Dk
Nchimbi anatakiwa kumuiga Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi
ambaye alijiuzulu akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani baada ya kutokea
mauaji, akijiuzulu atajijengea heshima tofauti na sasa kwani wananchi
wamesikitishwa na mauaji hayo,” alisema Lissu.
Mwanasheria wa
Chadema, Mabere Marando alidai kwamba kuna mkakati uliowekwa na Serikali
wa kukidhoofisha Chadema baada ya kuonekana kwamba ni tishio kwa CCM.
Mbali
na Chadema, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), pia
limesema halina imani na kamati hiyo likisema imekuwa kawaida kwa
Serikali kuunda tume ambazo hazileti ripoti kwa wananchi.
“Tume
zimekuwa zikiundwa bila faida yoyote, huku zikipewa muda kuchunguza
yaliyotokea lakini matokeo yake huwa hakuna ripoti wanayorudisha,”
alisema Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya.
Kaaya alisema
tume zimekuwa zikiundwa na kuigharimu Serikali fedha nyingi za walipa
kodi, lakini ripoti zake zinaendelea kuwa siri.
Imeandikwa na Habiel Chidawali, Dodoma, Hamida Sharrif Morogoro, na Tumaini Msowoya, Iringa na
Lasteck Alfred na Juliana Malondo.
0 Comments