Rais
Dk. Jakaya Kikwete akizungumza na Mwenyekiti wa Alliance for a Green
Revolution in Africa Dk. Kofi Annan (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa
Bill and Melinda Gates, Bibi Melinda Gates wakati wa ufunguzi wa Mkutano
wa Kimataifa wa” Africa Green Revolution Forum 2012,” uliofanyika
katika Ukumbi wa Ngurdoto Mountain Lodge Mjini Arusha.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya
Kikwete Septemba 27, 2012, amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Taasisi
ya Bill and Melinda Gates, Bi. Melinda Gates. Katika mazungumzo hayo
yaliyofanyika Club House, kwenye Hoteli ya Ngurdoto, mjini Arusha, Rais
Kikwete na Bi. Gates wamezungumzia masuala mbalimbali na hasa kuhusu
jinsi taasisi hiyo inavyoweza kuisaidia Tanzania hasa katika maeneo ya
kilimo na afya ya akinamama.
Rais Kikwete amemwomba Bi. Gates kuangalia jinsi ya kuisaidia
Tanzania kuanzisha taasisi ya kufutilia utekelezaji wa mipango, program
na maamuzi yote ya Serikali kuhusu mageuzi ya kilimo katika Tanzania.
“Tuna mambo mengi na shughuli nyingi zinazoendelea katika sekta ya
kilimo. Tunafanya mengi, lakini lazima tuwe na uwezo wa kujua kila jambo
linalofanyika liko kwenye hatua gani na linakwenda kwa mafanikio ama
matatizo yapi,” amesema Rais Kikwete.
Taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation inasaidia taasisi ya
namna hiyo katika Ethiopia, nchi ambayo kilimo chake kinakua kwa
asilimia sita kwa mwaka. Naye Bi. Gates amemwambia Rais Kikwete: “Kama
hilo ndilo jambo mnalolitaka basi hakuna shaka kuwa sisi tutavutiwa na
jambo hilo.”
Bi. Gates yuko mjini Arusha kuhudhuria Mkutano wa Pili wa Taasisi ya
Mapinduzi ya Kijani katika Afrika (AGRA) ambao umefunguliwa leo na Rais
Kikwete kwenye Hoteli ya Ngurdoto. Akizungumza kwenye sherehe ya
ufunguzi wa mkutano huo, Bi. Gates amemwagia sifa Rais Kikwete
akimweleza kama kiongozi anayejali sana maslahi ya Tanzania na maslahi
ya Afrika.
Bi. Gates amesema kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza ambayo yeye na
mumewe, tajiri Bill Gates walitembelea miaka 19 iliyopita na tokea
wakati huo wameitembelea nchi hiyo mara nyingi zaidi kuliko nchi
nyingine yoyote ya Afrika. “Hata mwaka huu, hii ni mara yangu ya pili
kuja Tanzania.”
Ameongeza: “Naipenda na kuitembelea Tanzania siyo tu kwa sababu watu
wake ni wema na wakarimu sana, na wala siyo tu kwa sababu nchi yenyewe
inavutia sana, lakini hasa hasa kwa asababu Tanzania ni mfano usiokuwa
na kipimo wa maendeleo na inajali sana mtu ambaye nasi tunamjali sana –
mkulima.”
0 Comments