Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete
Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya
Mrisho Kikwete amewasili nchini Kenya Septemba 11, 2012, kuanza Ziara
Rasmi ya Kiserikali (State Visit) ya siku tatu ikiwa ni ziara yake ya
kwanza rasmi nchini humo ingawa amefanya ziara kadhaa za kikazi nchini
Kenya.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, Rais
Kikwete ambaye amefuatana na mkewe, Mama Salma Kikwete, amepokewa na
mwenyeji wake, Rais Mwai E. Kibaki na kwa mbwembwe zote za kiprotokali
zinazoambatana na ziara rasmi za kiserikali.
Baadaye mchana, Rais amekwenda Ikulu ya Kenya ambako ametia saini kitabu
cha wageni, akafanya mazungumzo ya faragha na Rais Mwai Kibaki kabla ya
kufanyika kwa Mazungumzo Rasmi ya Kiserikali kati ya nchi hizo mbili
majirani na wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete na ujumbe wake amekwenda kwenye
Chuo Kikuu cha Kenyatta ambako umepokewa na Waziri wa Elimu ya Juu,
Margaret Kamar, Mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mstaafu Onesmus Mutungi na
Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Olive Mugendi.
Kwenye chuo hicho ambacho Desemba 8, mwaka 2008, kilimtunuku Rais
Kikwete Shahada ya Uzamivu ya Heshima, amefungua rasmi Jengo la Shule ya
Ukarimu na Utalii ya Chuo hicho.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Shule hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa
utalii ni sekta muhimu sana katika chumi za nchi za Afrika Mashariki na
ambayo mchango wake unagusa maisha ya maelfu kwa maelfu ya wananchi wa
nchi za ukanda huo.
Rais pia amesema kuwa nchi hizo za Afrika Mashariki sasa zimekuwa ni
eneo lenye mvuto mkubwa katika nyanja ya utalii ambao unaweza
kuwaingizia wananchi na mataifa ya Afrika Mashariki mapato zaidi kama
changamoto zinazoikabili sekta ya utalii kwa sasa zitashughulikiwa
ipasavyo na kwa pamoja na nchi hizo.
Miongoni mwa changamoto ambazo Rais Kikwete amezitaja ni ukosefu wa
miundombinu ya kutosha kufanikisha kwa namna bora zaidi sekta ya utalii,
ukosefu wa juhudi za pamoja kuitangaza Afrika Mashariki kama eneo
muhimu la utalii, na umuhimu wa kuboresha kiwango cha usalama wa
watalii.
Aidha, Rais Kikwete amezielezea changamoto nyingine kuwa ni pamoja na
umuhimu wa kuwepo na viza ya pamoja ya utalii kwa nchi zote za Afrika
Mashariki, kuwepo kwa safari za ndege za kutosha kutoka kwenye mataifa
makubwa yanayozalisha watalii kwa wingi kuja Afrika Mashariki na umuhimu
wa kupungua kwa nauli za ndege za kuja Afrika Mashariki.
Leo jioni, Rais Kikwete anatembelea Taasisi ya Utatifi wa Kilimo ya
Kenya (KARI) ambako anatarajiwa kupokelewa na Waziri wa Kilimo wa Kenya,
Mheshimiwa Dr. Sally J. Kosgei na usiku atakuwa mgeni rasmi kwenye
Dhifa ya Kitaifa ambayo itaandaliwa na mwenyeji wake, Rais Mwai Kibaki.
Kesho, Rais Kikwete ataweka shada la maua kwenye Kaburi la Mwanzilishi
wa Taifa la Kenya, Hayati Jomo Kenyatta, kwenye Viwanja vya Bunge la
Kenya na kutembelea Kiwanda cha Maziwa cha Brookside Diary kwenye
Barabara ya Thika.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara yake, Rais Kikwete atatembelea Chuo cha
Taifa cha Ulinzi cha Kenya (National Defence College) kilichoko Karen,
Nairobi, ambako atapokelewa na Waziri wa Nchi wa Ulinzi, Yusuf Haji na
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Julius Karangi.
Baadaye, Rais Kikwete atakwenda kutembelea Kituo cha Magonjwa ya Moyo na
Kansa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan ambako atapokelewa na
Waziri wa Huduma za Matibabu, Anyang Nyong’o.
Baadaye jioni, Rais Kikwete ambaye anaongozana na kundi kubwa la Wafanya
Biashara wa Tanzania atashiriki chakula cha jioni ambacho ameandaliwa
na Jumuiya ya Wafanya Biashara ya Kenya.
0 Comments