MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe amesema kuuawa kwa mwandishi wa Habari wa Kituo
cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi katika mkutano wa chama
hicho mkoani Iringa ni njama za polisi kuzima mikutano yake ya kujinadi
kwa wananchi.
Akifungua Mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho
iliyokutana kwa dharura Dar es Salaam jana kujadili hali ya siasa
nchini, Mbowe alisema hakuna mkakati wowote utakaozima Operesheni ya
Chadema ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) nchini.
Mwangosi aliuawa
katika vurugu zilizotokea wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi
wa Chadema waliokuwa katika sherehe za uzinduzi wa tawi la chama hicho,
Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi.
Alisema
Chadema kimeshangazwa na kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukaa kimya
kuhusu kifo cha Mwangosi wakati ni tukio ambalo limegusa hisia za watu
wengi ndani na nje ya nchi.
“Chadema tumeshangazwa na ukimya wa
Rais Jakaya Kikwete ambaye ni kiongozi wa nchi na mwepesi wa kushiriki
katika matukio mbalimbali na msiba. Lakini hili la kifo cha mwandishi wa
habari lililogusa jamii nzima ndani na nje ya nchi na kuibua hisia
kali, hajatoa tamko hadi leo,” alisema Mbowe na kuongeza: “Viongozi
wa Serikali wakikaa kimya, wanasukuma polisi kuzuia mikutano ya Chadema.
Sisi tunasema, mkakati wowote wa kuzia Operesheni ya Vuguvugu la
Mabadiliko la Chadema hautafanikiwa.”
Mbowe alisema kwa sasa taifa
linakabiliwa na migogoro mbalimbali ikiwamo ya migomo ya walimu,
madaktari na hivyo mauaji haya ya raia yanayotokea katika mikutano ya
vyama vya siasa yanawafanya wananchi kukosa imani na Jeshi la Polisi.
Amshukia Tendwa, Dk Nchimbi Katika
ufunguzi huo, Mbowe pia aliwashutumu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk Emmanuel Nchimbi na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa kuwa
ofisi zao zimetumika kupotosha ukweli wa tukio na kudanganya umma wa
Watanzania.
Alisema kauli ya Tendwa ya kutishia kukifuta Chadema
ililenga kuvuruga hali ya amani na utulivu iliyopo nchini na kumtaka
akitaka kufanya hivyo aanze na chama tawala, CCM.
“Chadema si
chama cha mfukoni, kina wanachama zaidi ya milioni mbili, kauli ya
Tendwa inahatarisha usalama wa taifa, asiwe kibaraka wa CCM kwa kutoa
matamko yanayolinda chama tawala... Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko
(M4C) itaendelea,” alisema Mbowe.
Apongeza vyombo vya habari Mwenyekiti
huyo wa Chadema alipongeza juhudi na ujasiri wa waandishi wa habari
waliokuwapo Nyololo, ambako Mwangosi aliuawa, kwa kutoa habari za ukweli
alizodai kuwa zimekinusuru chama chake.
Alisema kama siyo habari
na picha zilizoonyesha ushahidi wa wazi, propaganda zingepotosha umma
juu ya vurugu zilivyotokea na kusababisha kifo cha mwandishi wa habari.
Katika
mkutano huo, baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu na Baraza la Udhamini
Chadema, walitoa machozi, baada ya kuonyeshwa picha za mnato na video za
matukio ya vurugu zilizosababisha kifo cha mwandishi huyo.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene ndiye aliyekuwa akifanya kazi ya kufafanua hatua kwa hatua matukio ya picha hizo.
0 Comments