Maandamano ya wanahabari leo

Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Neville Meena

Waandishi wetu

WAANDISHI wa habari wa mikoa mbalimbali nchini, leo wanatimiza azma yao ya kufanya maandamano ya amani ya kimyakimya nchi nzima kulaani kuuawa kwa mwenzao, Daud Mwangosi katika tukio lililotokea Septemba 2, mwaka huu.Mwangosi aliuawa kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu la machozi wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa Chadema waliokuwa katika uzinduzi wa tawi lao katika Kijiji cha Nyololo, Iringa.

Katika Mkoa wa Dar es Salaam, maandamano hayo yataanzia katika Kituo cha Televisheni cha Channel Ten na kuishia katika Viwanja vya Jangwani.


Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Neville Meena alisema jana kuwa maandamano hayo yataanza saa 2:00 asubuhi yakiwashirikisha waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari.


Awali, maandamano hayo yalipangwa kuanzia Channel Ten, Mtaa wa Jamhuri na kupita katika Mtaa wa Azikiwe, Barabara ya Bibi Titi hadi katika Viwanja vya Mnazi Mmoja. Kuhusu hilo, Meena alisema mabadiliko hayo yamefikiwa katika mkutano baina ya viongozi wa Tef na polisi.


Alisema mkutano huo ulitokana na uamuzi wa jeshi hilo wa jana asubuhi kuyapiga marufuku maandamano kwa madai kwamba hayakufuata taratibu.


Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema maandamano hayo yalikuwa yamezuiwa na Polisi Mkoa wa Ilala baada ya kuona taratibu zilikiukwa.

Hata hivyo, kamanda huyo alisema baadaye alilazimika kuitisha kikao na wawakilishi wa wanahabari hao na kukubaliana kuhusu mabadiliko hayo ya ratiba.


Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lazaro Mambosasa alidai kuwa yalikuwa yamezuiwa kutokana na barua kuchelewa kuwafikia. Barua hiyo ilifikishwa katika ofisi hizo Jumamosi.

Alisema ombi la ulinzi kwenye maandamano linapaswa kufika polisi kabla ya saa 48 ili lifanyiwe kazi, kanuni ambayo jukwaa hilo lilikuwa limekiuka.


“Tulisikia taarifa ya kuwepo kwa maandamano katika vyombo vya habari wakati kibali cha ombi la maandamano hayo bado hakijafika kwetu,” alidai Mambosasa. “Tulishangaa kufuatwa asubuhi na mmoja wa viongozi wa Tef kufuatilia kibali chao cha maandamano juu ya kupatiwa ulinzi wa askari. Lakini hadi tunaonana naye tulikuwa bado hatujapata barua yoyote ya kuomba kibali hicho.”


Juzi, Kaimu Mwenyekiti wa Tef, Theophil Makunga alisema waandishi watakaoshiriki maandamano hayo watavaa ama nguo nyeusi au watafunga vitambaa vyeusi mkononi ikiwa ni ishara ya kuomboleza na kulaani kuuawa kwa mwenzao.

Makunga alisema uamuzi wa kufanyika kwa maandamano hayo ulifikiwa katika kikao cha Jukwaa hilo kilichofanyika Jumamosi, Dar es Salaam.


Ziara ya JK yazuia maandamano Arusha

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa

Arusha, Claud Gwandu alisema Polisi imewazuia kufanya maandamano hayo kwa kisingizio cha ziara ya Rais Jakaya Kikwete.


Gwandu alisema maandamano yao ni ya amani na kwamba hayajapangwa kufika eneo ambalo Rais au mkutano wake utafanyika.“Tunakutana kujadiliana lakini polisi wamezuia wakitaka tupange siku nyingine kwa vile anasema askari wengi wa ulinzi watakuwa katika mkutano wa Rais na ziara yake,” alisema Gwandu.


Mikoa mingine

Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakar Karsani alisema maandalizi katika klabu mbalimbali mikoani yamekamilika isipokuwa Ruvuma.


Alisema katika mkoa huo, UTPC imeagiza kusitishwa kwa maandamano hayo ili kupisha maandamano ya Chadema.

“Tumewaagiza waandishi kusitisha maandamano yao kupisha maandamano ya Chadema, kwani hatuwezi kuyachanganya na yale ya vyama vya siasa, hivyo wao wataandamana siku nyingine,” alisema.


Alisema tofauti na Mkoa wa Ruvuma, Mkoa wa Rukwa polisi ilizuia waandishi kuandamana kwa madai kwamba taarifa ilipaswa kutolewa saa 48 kabla ya kuandamana.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Shija Felician alisema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika.Alisema waandishi wa Zanzibar walikuwa katika maandalizi kwa ajili ya kufanikisha maandamano hayo.


Polisi wahaha

Katika hatua nyingine, askari wanne kati ya watano waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji hayo wameachiwa huru.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa kuachiwa kwa askari hao kumekwenda sambamba na polisi kufanya jitihada za kumnusuru mtuhumiwa aliyebaki ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji.

Habari hizo zimeeleza kuwa, baada ya kukamatwa Jumatatu na kuhojiwa kwa siku tatu, askari hao waliachiwa na kuruhusiwa kurudi mikoani kwao.


“Walihojiwa na baadaye kuruhusiwa kurudi, lakini yule aliyeonekana kumlipua mwandishi huyo kwa bomu ambaye ameonekana kwenye vyombo mbalimbali vya habari anaendelea kushikiliwa,” kilidokeza chanzo cha habari ndani ya polisi.


Mmoja wa watuhumiwa hao walioachiwa alisema anamshukuru Mungu kwa kusikiliza kilio chake hata akaachiwa na kuruhusiwa kurejea kwenye kituo chake cha kazi.


Alipoulizwa nini kinaendelea kwa mwenzao aliyebaki alijibu: “Ninachojua ameitwa mwanasheria wetu wa (polisi) kuangalia uwezekano wa kuifanya kesi hiyo iwe ya man slaughter (kuua bila kukusudia) badala ya murder (kuua kwa kukusudia). Ila alitakiwa kufikishwa mahakamani leo.”


Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi kuchunguza kifo cha mwandishi huyo, jana ilikutana na waziri huyo kupata maelekezo ya awali.

Dk Nchimbi aliunda kamati hiyo inayoongozwa na Jaji Stephen Ihema na kuipa hadidu sita za rejea katika utekelezaji wa majukumu yake.


Tendwa: Polisi walikosea kuizuia Chadema Iringa

Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa amesema polisi walifanya makosa kukiruhusu CCM kufanya kampeni katika Jimbo la Bububu, Zanzibar na kukizuia Chadema, kufanya ufunguzi wa matawi yake Iringa.

Mbali na hilo, Tendwa alisema ataibadili sheria ya utoaji vibali vya kufanya mikutano ya vyama vya siasa kutoka polisi na kutolewa na ofisi yake ikiwa wadau watapendekeza hivyo na Bunge kuridhia mabadiliko hayo.

Tendwa alitoa kauli hiyo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki alipokuwa akichangia mada kuhusu ‘ongezeko la mauaji katika mikutano ya siasa ni kukua kwa demokrasia?’ katika kituo cha Televisheni cha ITV.

Msajili huyo alisema sheria hiyo inaweza kubadilishwa na kumpa mamlaka ya kutoa vibali, endapo wadau watakuwa na kauli moja.

“Unakuta chama kinaomba kufanya mkutano wiki mbili kabla, lakini majibu hayatolewi kwa wakati kitendo ambacho kinasababisha kurudisha nyuma demokrasia.”


Alisema polisi ni moja na haitakiwi kujichanganya katika utoaji wake uamuzi. Alisema CCM iliruhusiwa kufungua kampeni zake Bububu na Chadema kuzuiwa kuandamana kwa kile kilichodaiwa kuwa Sensa ya Watu na Makazi ilikuwa ikiendelea, jambo alilosema ni makosa kwa kuwa kilichokuwa kikifanyika bara (sensa) na visiwani kilikuwa kikiendelea.


Hata hivyo, Tendwa alisema kuwa mara baada ya mauaji kutokea maeneo tofauti nchini kumekuwapo na matamko mbalimbali yanayotolewa na watu na taasisi bila kuwapo  hitimisho lake, hivyo ameandaa mjadala kuangalia eneo lenye makosa katika demokrasia ya Tanzania.Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema polisi imekuwa ikisababisha mauaji ya wananchi wasio na hatia.


Sungusia alisema mfumo wa polisi umepitwa na wakati na kinachotakiwa hivi sasa ni kufanyika kwa mabadiliko ya kuwaandaa askari hao ili wawatumikie wananchi na si kuwaua.SPC yataka RPC

Iringa akamatwe


Kwa upande wake, Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), kimeiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kumkamata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda na kumuunganisha na polisi wenzake kwenye mauaji ya kinyama ya Mwangosi.


Felician alisema yaliyofanyika jana mjini Kahama amedai kama Serikali ilimkamata Abdallah Zombe ambaye Cheo chake ni sawa na Kamuhanda kwa nini yeye asikamatwe ambapo kosa lake lina ushahidi wa kutosha kwamba alihusika kwa namna nyingine.


Mwaka 2007 Serikali ilimkamata aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya Jinai mkoani Dare Es Salaam, Zombe baada ya vijana wake kufanya mauaji ya wafanyabiashara watatu kwa maagizo yake lakini baadaye aliaachiwa na mahakama kosa ambalo halikuwa na ushahidi wa kutosha tofauti na la RPC Kamuhanda ambaye Mwandishi aliuawa yeye akishuhudia.


Mwenyekiti huyo alisema anashangaa Serikali kutumia gharama ya kuunda tume huku wauaji wakiongozwa na RPC huyo wanafahamika kwenye picha mbalimbali wanaonekana ambapo kwenye kesi ya Zombe aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani hakuna picha iliyoonekana polisi wakiua wafanyabiashara hao.


Alisema RPC Kamuhanda hawezi kukwepa kwamba hakuhusika na Mauaji hayo kutokana na mashuhuda mbalimbali waliokuwepo kwenye eneo la tukio ambao wengi wao walidai walithubutu hata kumfuata kwenye gari lake wakimtaka awazuie polisi wake wasimuue mwandishi huyo lakini ilidaiwa alipandisha kioo cha gari na kufunga kabisa na kuashiria kwamba hakuwa tayari kumsaidia mwandishi huyo asiuawe.


Felician alisema ili Watanzania wajue haki imetendeka vizuri bila kuonea polisi wadogo, RPC naye akamatwe na kuunganishwa kama mmoja wa watuhumiwa kwa mauaji hayo kwa kuwa polisi wadogo hupokea amri kutoka kwa wakubwa na wameua mbele yake hivyo naye anahusika .


Septemba 2, mwaka huu tasnia ya habari ilipata pigo kubwa kwa kuuawa mwandishi wa habari na wanaodhaniwa kuwa ni polisi waliokuwa wakidhibiti mkutano wa CHADEMA mkoani Iringa hali ambayo imebeba uzito mkubwa kwa nguvu kubwa iliyotumika na polisi kwa kumdhibiti mwandishi mmoja wa habari ambaye silaha yake ni kamera na kalamu.


Katika mauaji hayo askari watano walikamatwa na leo chama hicho cha waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga kitafanya maandamano makubwa ya amani kulaani mauaji hayo na kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Umoja wa Vilabu vya waandishi wa Habari Tanzania, Abubakari Karsani maandamano hayo yatafanyika nchi nzima.


_

Imeandikwa na Frederick Katulanda, Aziza Masoud, Pamela Chilongola, Zaina Malongo na Ibrahim Yamola.

Post a Comment

0 Comments