KAMANDA wa Kanda Maalum ya Polisi Mkoa wa Dar
es Salaam, Suleiman Kova amesema jeshi la Polisi linalifanyia kazi
tuhuma za utapeli unaomhusisha mke wa kigogo wa jeshi hilo na kwamba leo
litatoa taarifa.
Mbali na tukio hilo, jeshi hilo litatoa taarifa
za uchunguzi za majambazi yaliyopora mamilioni ya fedha kwenye Benki ya
Commercial Bank of Afrika (CBA) lililotokea Alhamisi iliyopita.
Kamanda Kova alisema jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na Mwananchi kwa simu baada ya kutakiwa kuzungumzia matukio hayo.
“Ninayafanyia
kazi mambo mliyoyaandika leo kwenye Mwananchi, nitatoa taarifa kesho
pamoja na upelelezi wa majambazi yaliyoiba mamilioni ya fedha katika
benki ya CBA unavyoendelea,” alisema Kova.
Alisema masuala yote hayo atayatoa kwenye mkutano na waandishi wa habari unaotarajia kufanyika leo.
Jana,
gazeti hili liliandika habari za watu 120 wenye elimu ya chuo kikuu
waliodai kutapeliwa mke wa mmoja wa makamishna wa jeshi la Polisi
waliopo makao makuu kwa kuchangishwa zaidi ya Sh100 milioni.
Walichangishwa
fedha hizo kwa ajili ya kufanyiwa mpango wa kupata ajira katika Idara
ya Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) lakini baadaye ilikuja kubainika kwamba ulikuwa utapeli.
0 Comments