IMEKUWA
kawaida sasa kuona habari nyingi zinazochapishwa au kutangazwa na
vyombo vya habari kuhusu Jeshi la Polisi nchini, kwa kiasi kikubwa
zimekuwa hazionyeshi taswira nzuri kuhusu jeshi hilo. Hali hiyo siyo tu
imethibitishwa na matukio ya kila siku hapa nchini, bali pia na tafiti
na tathmini mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa kila mwaka na taasisi
kadhaa zinazoheshimika za hapa nchini na nchi za nje. Tafiti na tathmini
hizo zimeonyesha, kwa mfano kwamba jeshi hilo, mbali na Mahakama
linaongoza kwa vitendo vya rushwa.
Nyingi ya taasisi hizo za
kitafiti, ikiwamo Transparency International ya Marekani zimesema,
tofauti na taasisi nyingine zilizokubuhu katika vitendo vya rushwa kama
ilivyo Mahakama, jeshi hilo pia hutumia mabavu, mateso na vitisho katika
kudai rushwa. Na kama hiyo haitoshi, pia taasisi kadhaa za haki za
binadamu, ikiwamo Amnesty International ya Uingereza zimefanya tafiti na
kutoa ripoti za kila mwaka zinazoonyesha kwamba jeshi hilo ni mkiukaji
mkubwa wa haki za binadamu.
Hiyo ndiyo taswira halisi ya
jeshi hilo katika nchi yetu. Hivyo, vyombo vya habari vinaporipoti
habari zenye kuonyesha taswira hasi ya jeshi hilo, havifanyi hivyo kwa
lengo la kulipaka matope, isipokuwa kuwajulisha wananchi kuhusu mwenendo
wake usiofuata maadili na weledi, ili wazishinikize mamlaka husika
zifanye mabadiliko stahiki kwa kulisafisha jeshi hilo katika ngazi zote
za uongozi. Ni jambo la ajabu kuona Jeshi lililokuwa la mfano barani
Afrika baada ya Uhuru wa nchi yetu, kwa maana ya kuwalinda wananchi na
mali zao na kuwa kimbilio la wanyonge, linageuka kuwa adui mkubwa wa
wananchi kwa kuwatisha, kuwatesa, kuwaua, kuuza haki zao na kuwadai
rushwa.
Hata vyombo vya habari vingejitahidi kiasi gani
kuisafisha, kuiremba na kuipodoa sura ya jeshi hilo katika hali lililomo
sasa hakika isingewezekana, kwani sura hiyo imechafuka kiasi cha
kutosafishika na kutorembeka tena. Habari za askari polisi kufanya
mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, au kushiriki katika mitandao ya wizi,
uporaji na ujambazi, au kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya,
usafirishaji wa binadamu, utapeli na uhalifu mwingine wa kutisha ndizo
habari zinazotoka katika jeshi hilo kwa wingi.
Hatuoni jinsi
jeshi hilo la polisi linavyoweza kuendelea kufanya kazi katika hali na
mazingira hasi lililomo hivi sasa kutokana na kupoteza sifa ya kuwa
Jeshi la Polisi. Kama wananchi wamefikia hatua ya kupaza sauti zao kwa
pamoja na kusema jeshi hilo ni adui yao namba moja, inawezekana kweli
askari wake wakavaa sare za jeshi hilo na kutembea kifua mbele kama
walinzi wa raia na mali zao? Hivi wanajisikiaje sasa wanapopita mitaani
na kusikia raia wakiguna na kuwabeza tofauti na zamani walipokuwa
kimbilio lao?
Hoja tunayoijenga hapa ni kwamba jeshi hilo
limeacha njia lililotumwa na waasisi wake kuifuata. Jeshi hilo
limechafuka na linanuka, hivyo tunadhani njia pekee iliyobaki ni
kulibomoa na kulisuka upya kwa kuwafukuza na kuwastaafisha wale wote
waliolifikisha hapa lilipo. Kwa kuzingatia ukweli kwamba siyo askari
wote waliomo katika jeshi hilo ni wala rushwa, wezi, majambazi au
wauaji, ingefaa ufanyike mchakato wa kura za maoni na za siri jeshi humo
ili askari waovu watambuliwe kwa majina.
Zoezi hilo linaweza
kuendeshwa na tume huru itakayoteuliwa na Rais au Bunge. Hata hivyo,
yafaa tutambue kwamba kupitisha fagio la chuma pekee hakutoshi kama
Serikali haitawaengua askari vihiyo, ili vijana wasomi na wenye
uadilifu, ambao wamejaa mitaani bila ajira wachukue nafasi zao.
Tunahitaji jeshi jipya la polisi lenye uadilifu na lililo rafiki wa
raia, linalotambua na kuheshimu haki za msingi za kiraia na ambalo
mikono ya askari wake haina harufu ya damu ya wananchi waliouawa bila
hatia.
0 Comments