Dk. Emmanuel Nchimbi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Waandishi Wetu
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi
ameunda kamati ya watu watano kuchunguza mauaji ya Mwandishi wa Habari
wa Kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi. Akitangaza kamati hiyo Dar es
Salaam jana, Dk Nchimbi aliwataja wajumbe wake kuwa ni Jaji Mstaafu,
Steven Ihema ambaye atakuwa Mwenyekiti na Mwakilishi wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga.
Wajumbe wengine ni
Mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, Mtaalamu
wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema
Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu. Mwangosi alifariki
Septemba 2, mwaka huu baada ya kupigwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni
bomu wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti wafuasi wa Chadema. “Kamati
hii nataka inipe majibu ndani ya siku 30 na kama utaalamu utakuwa
hautoshi tutaomba msaada nje,” alisema Dk Nchimbi.
Alisema kamati
hiyo itasaidia kujibu maswali sita ambayo hivi sasa hayana majibu
kutokana na tukio hilo. “Tuna maswali sita ambayo mimi sina majibu yake.
Swali la kwanza tunataka kujua nini chanzo cha kifo cha Daudi? Pili
tujue ni kweli kwamba kuna uhasama kati ya polisi na waandishi Iringa?”
alisema Dk Nchimbi na kuongeza: “Tatu tujue kama ni kweli kuna orodha ya
waandishi watatu wa kushughulikiwa Iringa? Nne kama nguvu zilizotumika
zilistahili? Tano kama kuna utaratibu wa vyama vya siasa kukata rufaa
dhidi ya uamuzi wa polisi? Mwisho kujua uhusiano wa Jeshi la Polisi na
vyama vya siasa ukoje?”
Dk Nchimbi alisema, sheria lazima
zifuatwe kwani nchi ikiingia kwenye matatizo, Serikali haitaweza
kuwaeleza wananchi kwamba ndicho kitu kinachotakiwa... “Hatutaki tuwe na
vita vya wenyewe kwa wenyewe.”
Katika hatua nyingine, Waziri
Nchimbi alisema anashangazwa na kutohojiwa kwa Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa kutokana na ujumbe aliomtumia Inspekta Jenerali wa
Polisi (IGP), Said Mwema siku moja kabla ya tukio.
Chadema
wamwangukia JK Chadema kimemwomba Rais Jakaya Kikwete kuwasimamisha
kazi Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Kamishna
Paul Chagonja, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda
pamoja na askari saba walioshiriki kwenye vitendo vya mauaji ya Mwangosi
ili kupisha uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
wa Chadema, John Mnyika alisema kuwasimamisha kazi viongozi hao
kutasaidia kufanyika kwa uchunguzi wa haki, jambo ambalo linaweza
kurudisha imani ya wananchi kwa Serikali yao. “Ni tukio la kinyama
kwelikweli ambalo limeitia doa Serikali, ili waweze kujisafisha,
tunamwomba Rais Kikwete kutumia mamlaka aliyonayo kwa kuwachukulia hatua
kali wahusika, jambo ambalo linaweza kurudisha imani kwa wananchi,”
alisema Mnyika.
Alisema kuwajibika kwao kutasaidia kupata taarifa
sahihi kuhusu kifo hicho kwa sababu wataweza kumtambua kiongozi
aliyewatuma askari hao kufanya mauaji hayo ili aweze kuchukuliwa hatua.
Chama
cha Wananchi (CUF) kimelitupia lawama Jeshi la Polisi kuwa limehusika
na vurugu zilizotokea Iringa na kusababisha kifo cha Mwangosi.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake, Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, Jeshi hilo linastahili kubeba
lawama za vurugu na kifo cha mwandishi huyo kwa kuwa lilishindwa
kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa baina yao na Chadema.
“Kwa
mtazamo huu, CUF tunaona wanaopaswa kubeba lawama hii ni Jeshi la Polisi
na wala si (Chadema), kwani kama tulivyoeleza awali, ilitosha kuheshimu
makubaliano yaliyofanyika baina yao na hata kama kulitokea vurugu
haikuhitajika kutumika nguvu kubwa kiasi hiki,” alisema Profesa
Lipumba.
Tucta Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania
(Tucta) limeitaka polisi kubuni mbinu mpya za kisasa katika matumizi ya
silaha wakati wa kukabiliana na vurugu zinazotokana na harakati za
kisiasa.
Akitoa tamko hilo Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu
wa Tucta, Hezron Kaaya alisema kama kweli mauaji hayo ya mwanahabari
yamefanywa na askari polisi, jeshi hilo linaipeleka nchi pabaya.
“Ikumbukwe
kuwa matukio yanayoonekana madogo leo ndiyo ambayo baadaye huzaa
machafuko makubwa katika nchi. Haya tumeyashuhudia katika nchi nyingine
na kamwe Tucta hatupendi nchi yetu ifike huko. Tunalaani mauaji hayo na
tutapenda kuona uchunguzi wa kina na ulio huru unafanyika na taarifa
kamili ya tukio hilo itolewe kwa umma,” alisema Kaaya.
Habari hii imeandikwa na Boniface Meena, Zaina Malongo, Patricia Kimelemeta, Geofrey Nyang'oro na Magreth Munisi.
0 Comments