YAKUTANA LEO DAR, MTEI AMTAKA KIKWETE ATOE TAMKO KUHUSU MAUAJI HAYO
Fidelis Butahe
KAMATI Kuu (CC) Chadema inakutana leo katika kikao
chake cha dharura, kujadili hali ya siasa nchini na mauaji yaliyofanywa
na Jeshi la Polisi katika mikutano yake, yakiwamo ya mwandishi wa Kituo
cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi.
Kikao hicho
kitakachoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kitatoa
uamuzi wake juu ya vitendo vinavyofanywa na polisi na Serikali, hasa
baada ya Rais Jakaya Kikwete kushindwa kutoa tamko lolote hadi sasa.
Taarifa
iliyotolewa na chama hicho jana ilieleza kuwa vitendo vinavyofanywa na
polisi ni kinyume na Katiba ya nchi na kudai kwamba, lengo la Serikali
ya CCM ni kuzima Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), inayofanywa
na chama hicho.
Kikao hicho kinafanyika ikiwa wiki moja imepita,
tangu polisi walipodaiwa kumuua Mwangosi aliyekuwa mwandishi wa Kituo
cha Televisheni, Channel Ten mkoani Iringa.
Mwangosi aliuawa na
mlipuko unaoaminika kuwa ni wa bomu, ambao ulisambaratisha vibaya viungo
mbalimbali vya mwili wake Septemba 2 mwaka huu, katika eneo la
Nyololo, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, wakati akiripoti tukio la
Chadema kufungua matawi yake.
Inadaiwa kuwa bomu hilo lilipigwa na polisi waliokuwa wakijaribu kuusambaratisha mkutano wa Chadema.
Mwangosi alizikwa siku moja baadaye katika Kijiji cha Kasoka kilichoko wilayani Rungwe, Mbeya.
Hadi
sasa askari watano wa Jeshi la Polisi akiwamo anayetuhumiwa kumlipua
Mwangosi kwa bomu, wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa na jeshi hilo
mkoani Iringa.
Kukamatwa kwa askari hao kulifanyika siku moja
baada ya kubainika kuwa askari kadhaa walioendesha operesheni dhidi ya
wafuasi wa Chadema mkoani Iringa na kusababisha kifo cha Mwangosi,
walitoka mikoa ya Dodoma, Mbeya na Morogoro.
Taarifa hiyo ya
Chadema ilieleza kuwa mbali na Mwangosi, pia hivi karibuni mjini
Morogoro polisi walisababisha mauaji ya mfuasi wa chama hicho, Ali
Singano (Zona) baada ya kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi
wao waliokuwa wakijiandaa kuwapokea viongozi wa kitaifa waliokuwa na
ratiba ya kufanya mkutano wa hadhara mjini humo.
“Baada ya tukio
hilo chama kilitoa kauli kumtaka Rais Jakaya Kikwete aagize kutumika kwa
Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) ili kubaini chanzo na kuondoa
utata wa kifo cha kijana huyo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na
kuongeza:
“Hivi karibuni yametokea mauaji ya Mwangosi, chama
kilimtaka Rais Kikwete aagize kufanyika uchunguzi huru kupitia tume ya
kimahakama kwa kuwa katika tukio hilo, hakukuwa na utata kuwa mwandishi
huyo aliuawa na polisi.”
Ilieleza kuwa ilitakiwa ufanyike
uchunguzi katika matukio hayo, ili kubaini vitu vya ziada, kama vile
ukiukwaji mkubwa wa Katiba, haki za binadamu na sheria za nchi na
aliyetoa amri za mauaji hayo.
Ilieleza kuwa chama hicho kilipinga
kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi kwa sababu iliundwa kinyume cha sheria ya tume za uchunguzi.
“Lengo
la kuundwa kwa kamati hii ni kufunika mambo na kurejesha uhusiano wa
Serikali na vyombo vya habari, badala ya kutafuta ukweli. Kwa mara
nyingine tena chama kilimtaka Rais Kikwete aunde tume huru ya uchunguzi
kwa mujibu wa sheria ili kweli ujulikane,” imeeleza taarifa hiyo na
kuongeza:
“Chadema kiliahirisha Operesheni ya Vuguvugu la
Mabadiliko (M4C) mjini Iringa, kikisisitiza kauli yake ya kumtaka Rais
Kikwete kuingilia kati, kuhakikisha analinda Katiba ya nchi inayotambua
haki ya kuishi.”
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kutokana na Rais
Kikwete kuwa kimya hadi sasa kuhusu matukio ya mauaji yanayofanywa na
polisi, Chadema kimeamua kuitisha mkutano wa dharura, kujadili hali hiyo
na kutoa uamuzi dhidi ya polisi.
“Tutatoa uamuzi wa hatua zaidi
za kuchukua dhidi ya Jeshi la Polisi na Serikali inayoongozwa na CCM,
kwa manufaa ya taifa letu na Watanzania wote kwa ujumla,” ilieleza
taarifa hiyo.
Mtei Naye Moses Mashalla kutoka
Arusha, anaripoti kuwa mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei amemtaka Rais
Kikwete ashtuke na kusema jambo kuhusu mauaji ya Mwangosi.
Akizungumza
akiwa nyumbani kwake Tengeru nje kidogo ya Jiji la Arusha, Mtei
alishangaa ukimya wa Rais Kikwete baada ya mauaji hayo, akisisitiza
kwamba ukimya wake utaifanya nchi isitawalike.
“Ni lazima Rais
Kikwete aseme jambo. Ni lazima kama mkuu wa nchi ashtuke, mimi nashangaa
ukimya wake juu ya mauaji haya, nchi hii haitaweza kutawalika,” alisema
Mtei.
Hata hivyo, alibainisha kuwa taifa haliwezi kuwa na polisi
wanaolenga vichwa vya watu na kuwaua badala ya kuwalinda wao na mali
zao.
Alitoa wito kwa Serikali kuwanyang’anya polisi wote nchini
silaha za moto na kuwakabidhi silaha za plastiki, maji ya kuwasha,
virungu pamoja na pingu pekee kwa kuwa wameshindwa kudhibiti matumizi
ya silaha za moto.
Mtei, aliyewahi kuwa gavana wa Benki Kuu
nchini, alitoa wito kwa askari wote waliohusika na mauaji ya mwandishi
huyo sanjari na vigogo wa Jeshi la Polisi waliotoa amri ya kutekeleza
mauaji hayo kujiuzulu mara moja kwa kuwa taifa linakoelekea ni kubaya.
“Hatuwezi
kuwa na polisi wanaolenga vichwa vya watu, taifa linaelekea kubaya.
Polisi hawa wanyang’anywe silaha za moto kwa kuwa hawajui matumizi
yake,” alisisitiza Mtei.
0 Comments