BAADA ya kimya cha muda mrefu, baba mzazi wa
kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka,
amekubali kuzungumzia sakata la mwanaye kutekwa, kuteswa, kutibiwa na
hatimaye kurejea nchini akisema kwamba kupona kwake ni neema za Mungu,
huku akiishutumu Serikali kuwa imewatelekeza Watanzania.
Hii ni
mara ya kwanza kwa baba huyo, Ulimboka Mwaitenda kuzungumza tangu
mwanaye alipotekwa, kuteswa na baadaye kutupwa katika Msitu wa Pande,
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
“Naishangaa Serikali hii
ambayo wananchi wanapigwa na kuuawa bila makosa. Nakumbuka kiongozi
aliyeipenda Tanzania ni mmoja na ameshatangulia mbele za haki,” alisema
akimaanisha Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Mwaitenda alitoa
kauli hiyo jana baada gazeti hili kumtafuta ili azungumzie habari
zilizoenea nchini kwamba mwanaye, amepata kazi nje ya nchi.
Kuhusu
madai hayo, Mwaitenda alikanusha akisema kuwa mtoto wake hawezi kwenda
nje ya nchi bila yeye kufahamu... “Pengine ana mipango hiyo, lakini mimi
sijui wala sijasikia, lakini atakwenda nje ya nchi kufanya nini? Hizi
habari hizo ndiyo nazisikia kwako kwa mara ya kwanza eti Ulimboka
anataka kwenda nje ya nchi? Akafanye nini alichokosa hapa Tanzania!”
Wakati
mwandishi akiingia nyumbani kwa Mwaitenda, Ubungo Kibangu, Dar es
Salaam, alipishana na Dk Ulimboka akiwa kwenye gari na wenzake, wanne.
Hata hivyo, hakufanikiwa kuzungumza naye.
Kuhusu tukio la kutekwa,
kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Pande, Mwaitenda alisema: “Mpaka
sasa, tumeiona kazi ya Mungu, ile ni neema ya Mungu kwa sababu wewe
uliona wapi mtu akapigwa namna ile halafu akapona kama si kwa neema tu.”
Alisema
alimkanya mtoto wake huyo aachane na masuala ya migomo na siku chache
baada ya onyo lake ndipo akatekwa na kujeruhiwa vibaya.
“Nilimkanya
kabisa kuhusu mambo ya migomo hasa baada ya kuniambia kuwa amechaguliwa
kuwa msemaji mkuu wa madaktari wenzake na kwa bahati mbaya ndiyo
yakatokea hayo yaliyotokea,” alisema.
Alielezea kushangazwa kwake
na watu waliompiga mtoto wake akisema, hajui walikuwa wanataka nini.
Alisema hakuwa na uhasama na mtu yeyote kuanzia kazini kwake hata kwa
marafiki zake.
“Mpaka sasa nashindwa kuelewa kwa nini waliamua
kumpiga, kwa sababu kwa ninavyomjua Steven, hajawahi kuwa na ugomvi na
mtu tangu anasoma shule ya msingi mpaka anamaliza chuo kikuu. Sijawahi
kupata mashtaka kuwa amegombana na mtu. Nashangaa haya yanayotokea leo.”
Akitoa
wasifu wa mwanaye huyo alisema tangu utoto wake, daktari huyo alikuwa
mtulivu na mwenye upeo wa hali ya juu. Alisema anasikitishwa mno na
yaliyompata akisema kwamba siku moja ukweli utawekwa wazi kwani siku
zote kazi za Mungu na kazi za shetani haziwezi kuchangamana.
“Kama
mafuta na maji, ukiyachanganya... mafuta yatakuwa juu na maji yatabaki
chini. Najua siku moja Mungu ataweka wazi ukweli,” alisema.
Kuhusu
afya ya Dk Ulimboka, Mwaitenda alisema ingawa yeye si daktari, lakini
anamwona mtoto wake kuwa yu mwenye afya na kuongeza kuwa hata mwanaye
huyo amekuwa akisema kwamba sasa ana afya njema.
Hali nyumbani kwa Mwaitenda Baada
ya kufika nyumbani kwa mzazi huyo wa Dk Ulimboka, mwandishi
alikaribishwa vyema na mzazi huyo ingawa alimtahadharisha kwamba endapo
angekutana na daktari huyo hapo au ndugu zake, wangemfukuza.
“Una bahati ungewakuta hapa watoto wangu tusingezungumza. Hata hawa mabinti zangu wakikukuta, hatutaendelea na mazungumzo....”
Hivyo
ndivyo ilivyotokea kwani baada ya kuelezea hayo, mabinti wake wawili
walitokea na mmoja akaanza kwa kusema... “Shikamoo Baba, umesharudi?
Huyu nani?”
Mzee Mwaitenda, kwa bashasha aliwatambulisha mabinti
hao... “ Huyu ni Florence... mwandishi wa Mwananchi...” Hata kabla
hajaendelea binti huyo na mwenzake walimshika mkono na kumwamuru atoke
nyumbani hapo mara moja.
“Haya dada toka, toka, mmeshindwa
kuandika kuhusu mwandishi mwenzenu aliyekufa (Daudi Mwangosi), mnakuja
kutufuata mpaka huku Kibangu.... mtazame miguu ilivyomchafuka kwa vumbi
kwa kushadadia ya watu, toka kabla sijakupiga makofi,” alisema mmoja wa
mabinti hao. Madai Dk Ulimboka kutoweka Rais
wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi ambaye alikuwa
karibu na Dk Ulimboka wakati wa mgomo wa madaktari nchini, alisema tangu
waonane aliporejea nchini kutoka Afrika Kusini, hajawasiliana tena.
“Hatujawasiliana
naye,” alisema Dk Mkopi na kusema kulingana na ukubwa wa tatizo
lililompata, hakuwa na mpango wa kumsumbua, bali kumwacha apumzike hadi
atakapokuwa amejisikia mwenyewe kurejea kazini.
Aliyekuwa kiongozi
wa jopo la madaktari waliomhudumia, Profesa Joseph Kahamba alisema,
hajawahi kuonana wala kuwasiliana na Dk Ulimboka tangu alipopelekwa
Afrika Kusini, Juni mwaka huu.
0 Comments