 |
Mkuu
wa Operesheni Sangara-Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) chama cha Chadema,
Benson Kigaila akiwa chini ya ulinzi katika gari la polisi mara baada ya
kukamatwa kwa viongozi na wanachama wa chama hicho katika eneo la
Msamvu Morogoro wakati wakiwasiri msafara wa Katibu Mkuu Taifa wa
Chadema na viongozi wengine kwa ajili ya mkutano wa chama hicho katika
Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
|
POLISI WATUMIA MABOMU KUWATAWANYA CHADEMA, MMOJA ADAIWA KUUAWA KWA RISASI,WAWILI WAJERUHIWA
Juma Mtanda na Hamida Shariff, Morogoro
VURUGU
kubwa zimezuka mjini Morogoro baina ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) na Polisi na kusababisha kifo cha mtu mmoja
anayedaiwa kuwa mfuasi wa chama hicho cha upinzani.Tukio hilo
lilisababisha taharuki kubwa katika eneo kubwa la Manispaa ya Morogoro,
huku wanachama na baadhi ya viongozi wa chama hicho wakionekana kuzagaa
katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya mjini na Hospitali ya Mkoa
alikopelekwa maiti huyo na polisi kwa lengo la kupata taarifa zaidi.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shillogile alithibitisha kutokea
kwa kifo hicho lakini akasema haijathibitishwa kwamba aliuawa kwa bomu,
risasi au ajali na kwamba jeshi hilo linafanya uchunguzi kujua chanzo
cha kifo chake.
Hata hivyo, alisema polisi walilazimika kutumia
risasi za moto kuwatawanya wafuasi wa Chadema baada ya chama hicho
kukaidi agizo lililowataka wasifanye maandamano.
Kifo hicho
kilitokea katika eneo la Msamvu ambako wafuasi hao walikusanyika,
wengine wakitokea Barabara ya Dar es Salaam na wale waliokuwa wakitokea
Barabara ya Dodoma, tayari kuwapokea viongozi wa kitaifa wa Chadema.
Mfuasi huyo aliyefahamika kwa jina la Ally Zona (38), Mkazi wa Kihonda ni mpigadebe kwenye Kituo cha Mabasi Msamvu.
Taarifa
za awali zilizolifikia gazeti hili, zilieleza kuwa Zona alifariki
dunia wakati polisi wakirusha mabomu ya machozi na risasi kuwatawanya
wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakijiandaa kuandamana na baadaye
kuhudhuria mkutano katika Uwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.
Tukio hilo lilitokea jana saa 7:30 mchana.
Ilivyokuwa
Baada
ya wafuasi hao kukusanyika Msamvu tayari kuanza maandamano, polisi
walitoa amri ya kuwataka watawanyike, lakini walikaidi hivyo kuamua
kurusha mabomu ya machozi na risasi hewani kuwatawanya kitendo ambacho
kiliwafanya wafuasi hao kutawanyika na kukimbia ovyo.
Kamanda
Shillogile alisema baada ya tukio hilo na taarifa za kifo cha mfuasi
huyo wa Chadema, ameamua kutuma askari kwenda katika chumba cha
kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa ili kushirikiana na madaktari
kuchunguza sababu za kifo hicho.
“Uchunguzi huo utabaini kama mtu
huyo amefariki kutokana na bomu, risasi au ajali kwani wakati wa vurugu
hizo watu walikuwa wakikimbia ovyo kwa kutumia magari na pikipiki,”
alisema Shillogile na kuongeza:
“Kutoka eneo lililokuwa na vurugu
hadi alipookotwa marehemu huyo, pana umbali kidogo kwa hiyo uchunguzi
huo ndiyo utakaoeleza ukweli.”
Alisema kuwa uchunguzi wa awali,
unaonyesha kwamba mwili wa Zona ulikutwa ukiwa unatoka damu kichwani
kutokana na jeraha ambalo haijafahamika limetokana na nini.
Hata
hivyo, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alidai kwamba kifo hicho
kimetokana na risasi aliyopigwa kichwani na siyo bomu... “Kwa kitendo
hicho polisi wanaonekana kuwa walifanya kusudi na walidhamiria kuua.”
Alisema
mwili wa marehemu hautazikwa mpaka uchunguzi wa kidaktari
utakapofanyika. Aliwataka walioshuhudia tukio hilo kujitokeza kutoa
ushahidi ili askari waliohusika wachukuliwe hatua.
Alisema Chadema kimemteua Mwanasheria wake wa Mkoa wa Morogoro, Aman Mwaipaya kushuhudia wakati uchunguzi huo ukifanywa.
Kauli ya Chadema
Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika baadaye jioni, Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kifo cha kijana huyo kinaongeza kasi
ya mapambano ya chama hicho dhidi ya ukombozi wa kweli.
Alimlaumu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa na Kamanda wa Polisi Wilaya kwa kuamrisha
askari wao kutumia nguvu dhidi ya wananchi wasiokuwa na silaha.
“Tuko
tayari kushirikiana na familia ya kijana huyo kwa ajili ya taratibu
zote za mazishi. Tutamzika kishujaa kwa kuwa alikufa akikipigania
chama,” alisema Dk Slaa.
Aliwataka wananchi kuonyesha uchungu kwa kifo cha mfuasi huyo kwa kutupa kadi za CCM na kuchukua za chama hicho cha upinzani.
Awali,
Mwaipaya alisema kifo cha mfuasi huyo kimesababishwa na polisi baada ya
kurusha mabomu ya machozi na kusababisha vurugu na taharuki kwa
wananchi pamoja na wanachama wa Chadema.
Alisema wakati wananchi
wakiwasubiri viongozi wa Chadema; Dk Slaa, John Mnyika, Halima Mdee na
Mchungaji Peter Msigwa, walikuwa hawafanyi vurugu zozote.
“Polisi ndio waliosababisha vurugu, baada ya kuanza kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi.
Nilishuhudia wakati marehemu (Zona) akidondoka,” alisema.
Viongozi wa Chadema mbaroni
Licha
ya Kamanda Shillogile kueleza kuwa hakuna kiongozi wa Chadema
aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo, taarifa zimeeleza kuwa jeshi hilo
linawashikilia viongozi wake kadhaa akiwamo Mkuu wa Operesheni ya
Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Benson Kigaila.
Kigaila na viongozi
wengine walikamatwa baada ya kufika Msamvu wakati jeshi la polisi
likiwa katika harakati za kuzuia mikusanyiko ya watu na kuwalazimisha
kushuka katika magari yao na kuwakamata.
Maandalizi ya polisi
kudhibiti maandamano ya Chadema yalianza majira ya saa 3:00 asubuhi kwa
kutumia Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ambacho kilionekana kikiwa na
magari yasiyopungua matano kikirandaranda katika mitaa mbalimbali ya
Morogoro.
Polisi hao walikuwa wakitangaza kuzuiwa kwa maandamano
hayo na kuwataka wananchi kutojitokeza kushiriki wakionya kuwa hatua za
kisheria zitachukuliwa kwa watakaokaidi.
0 Comments