Mzee
Paulo Mawezi maarufu kama Matonya akiwa na mwanae Elizabath wakiwa
katika Kijiiji cha Mpamantwa Tarafa ya Bahi Mkoani Dodoma. Picha hii
ilipigwa 2010 wakati alipokwenda kwa mapumziko ya sikukuu ya Krismas.
Picha na Maktaba
Habel Chidawali, Bahi
LICHA ya umaarufu mkubwa aliokuwa nao na
kufahamika katika miji mingi nchini, ombaomba Paul Mawezi maarufu kwa
jina la Mzee Matonya, amefariki dunia na kuzikwa katika mazingira ya
ufukara mkubwa.
Matonya alizikwa jana kijijini kwake Mpamantwa,
Wilaya ya Bahi, Dodoma akiwa amevishwa nguo moja nyeusi, huku mwili wake
ukibebwa na watu wasiozidi 20, waliotumia ngozi kuu kuu ya ng’ombe.
Matonya
aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kikohozi tangu Mei mwaka huu,
alifariki dunia juzi usiku na kuzikwa jana saa saba mchana mita tatu
kutoka katika nyumba yake ya tembe alimokuwa akiishi.
Ndugu na
jamaa zake wa karibu walisema Matonya ambaye umri wake unakadiriwa kuwa
zaidi ya miaka 90, hakuwahi kwenda kutibiwa hospitali kutokana na
ukosefu wa fedha.
Mwandishi wetu alishuhudia idadi ndogo ya
waombolezaji nyumbani kwa Matonya, huku watoto wake watatu waliokuwapo
msibani hapo kati ya watano aliowaacha hai, wakisema kuwa baba yao
amefariki kutokana na umaskini na ufukara.
“Hatukuweza kumpeleka
hata hospitali kupata vipimo kwani hatukuwa na uwezo wa kwenda mjini
Dodoma kutokana na kukosa hata nauli, ndiyo maana tumekuwa kimya hadi
Mungu alipomchukua,’’ alisema mmoja wa watoto hao, David Paulo.
Umaarufu wa Matonya
Umaarufu
wa Matonya ulitokana na staili yake ya kuomba kwa kulala chali
barabarani, huku akiwa ameinua kopo juu bila ya kujali jua au mvua.
Kwa
nyakati tofauti alipinga mpango wa Serikali wa kumrejesha kwao Bahi na
mara kadhaa alimweleza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusufu
Makamba kuwa yeye ni mtoto wa mjini hivyo asingemuweza. Aliingia Dar es
Salaam kwa mara ya kwanza Desemba 7, 1961.
Katika siku za karibuni, alikuwa gumzo kwa Serikali na viongozi huku akipachikwa jina la Komandoo na Kiboko ya Makamba.
Baada
ya kuondolewa Dar es Salaam, aliweka makazi yake mapya ya kuomba mkoani
Morogoro hususan eneo la Darajani, ambako aliendeleza staili ya kuomba
akiwa amelala chali na kuinua kopo juu kwa muda mrefu bila kuchoka.
Iliwahi
kuvuma kwamba ombaomba huyo alikuwa na utajiri mkubwa, jambo ambalo
mtoto wake mkubwa, Elizabeth Paulo alilipinga na kusema kwamba halina
ukweli na hakuacha chochote.
Mke wa Marehemu Paulina alisema
walitengana na Matonya zaidi ya miaka 37 iliyopita na wakati huo alikuwa
na mali nyingi (ng’ombe).
“Tulipotengana tu, mimi nilirudi kwetu
na watoto wangu walikuwa bado wadogo na bahati mbaya mdogo wake
aliyekuwa akitunza ng’ombe (wa Matonya) alifariki dunia na huo ukawa
ndiyo mwanzo wa kumaliza mifugo yote kwani watu waliwaiba wote,’’
alisema Paulina.
Matonya alirudi kijijini kwake Mpamantwa kwa
ajili ya mapumziko ya Krismasi Novemba, 2010 akitokea Morogoro kama
ilivyokuwa kawaida yake na tangu wakati huo hakurudi tena.
Makamba, Mashishanga wamlilia
Akizungumzia
msiba huo, Makamba ambaye alifanikisha mpango wa kumwondoa Matonya Dar
es Salaam, alisema amesikitishwa na kifo hicho cha mtu aliyemtaja kuwa
alikuwa rafiki yake mkubwa.
“Nasikitika nimempoteza rafiki mkubwa… Mimi nilimpenda lakini inaonekana Mungu amempenda zaidi,” alisema Makamba jana kwa simu.
Alisema
urafiki wao ulianzia pale alipomwondoa Dar es Salaam na kumrejesha
nyumbani kwao Dodoma, lakini baadaye akahamia Morogoro... “Alipokwenda
Morogoro (Matonya) alisema ‘naipenda CCM, lakini simpendi Makamba.’
Waandishi waliponifuata wakaniuliza nikasema mimi nampenda,” alisema
Makamba.
Alisema kauli yake ya kumpenda inathibitishwa na mkakati
wake wa kutaka kumwondoa katika mazingira ya dhiki na jua kali wakati wa
kuombaomba katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kumpeleka kwao Dodoma,
ambako angeweza kutulia na kuishi vizuri na ndugu zake.
“Alikwenda
huko, lakini kwa bahati mbaya kama Waswahili wasemavyo, mazoea yana
tabu, akarejea kwenye kazi yake mkoani Morogoro,” alisema Makamba.
Makamba
ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM kabla ya kustaafu,
alisema Matonya alikuwa mmoja wa makada wanaokipenda chama hicho tawala,
hivyo licha ya kusikitika kupotelewa na rafiki, pia anasikitishwa na
chama kumpoteza mmoja wa wakereketwa wake.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Mkoa wa Morogoro mstaafu, Stephen Mashishanga alisema, Matonya
alikuwa mzee maarufu na hakuwa mtu aliyependa makuu kwani kila
alipotakiwa kuondoka mjini alitii.
Alisema kifo chake
kimemsikitisha kama binadamu mwenzake hasa akikumbuka kuwa hakuwahi
kumnyanyasa, akisema alikuwa ombaomba aliyependa kukaa eneo moja na kila
aliyemwonea huruma alitoa sadaka yake.
“Alipotakiwa kuondoka,
aliondoka lakini baadaye alirudi mahali ambako kuna masilahi; Hata
ng’ombe hukimbilia mahali ambako anajua kuna nyasi za kutosha,” alisema
Mashishanga.
0 Comments