Wananchi waliokuwa wanaishi mabondeni
jijini Dar es Salaam na kuhamishiwa Mabwebande na Serikali kutokana na
mafuriko ya mvua za mwishoni mwa mwaka jana, wapo hatarini kupata
magonjwa ya milipuko baada ya vyoo vichache wanavyotumia kwa
kushirikiana kujaa na kutoa wadudu na mahema wanayoishi kuchanika.
NIPASHE Jumapili jana ilishuhudia vyoo hivyo vikiwa katika hali mbaya huku wakazi hao wakiendelea kuvitumia.
Imeshudia kaya 18 zikitumia vyoo viwili licha ya kaya nyingine kuwa na idadi kubwa ya watu.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema
changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni vyoo kujaa na mahema kuwa
katika hali mbaya baada ya kuchanika na kusababisha wadudu kuingia
ndani.
Mmoja wa wakazi hao, Fatuma Salim alisema vyoo hivyo kwa sasa vinatoa
wadudu aina ya funza na vimejaa mapema kutoka na idadi kubwa ya watu
kutumia choo kimoja.
"Kama unavyoona hapa huu upande una mahema 18 na vyoo vipo viwili na
mabafu yapo manne hivyo tukaamua kugawana wanaume watatumia choo chao na
wanawake kutumia choo chao ila tunaishi kwa nguvu za mungu kwani
magonjwa yapo nje nje," alisema.
Amina Mohamed alisema mbali na tatizo hilo pia hawapati huduma za afya
kwa wakati tangu kituo cha msalaba Mwekundu kilivyoondoka katika eneo
hilo miezi mitatu iliyopita.
Alisema hospitali wanayoitumia kwa ipo mbali na pia imekuwa ikifungwa mapema majira ya saa 8:00 alasiri.
Alisema bado wanaishi katika mazingira magumu licha ya serikali kuwapatia eneo zuri kutokana na kukosa huduma ya matibabu.
"Kwa wajawazito wanapata tabu pale wakishikwa uchungu kwani katika suala
la usafiri hakuna na ukiangalia hospitali ambayo tunapatiwa huduma
imekuwa ikifungwa mapema ni kweli serikali imetupatia eneo zuri ila bado
tunaishi katika mazingira magumu," alisema Mohamed.
Mohamed alisema mahema mengi yameanzwa kuliwa na mchwa hali ambayo
imewasababishia kujengea kwa udongo ili yasindondoke kwani bila kufanya
hivyo wataendelea kuishi katika mazingira magumu.
Alisema serikali iliwaahidi kuwaletea dawa kwa ajili ya kupulizia mchwa
hao ili wasiendelee kutafuna miti jambo ambalo halijatekelezeka mpaka
sasa.
Alisema waliahidiwa pia kuletewa dawa kwa ajili ya kupulizia vyoo hivyo
ili kujiepusha na magonjwa lakini mpaka sasa ni zaidi ya miezi miwili
hawajapatiwa huduma hiyo.
Naye Zephania Mahega, alisema kuna baadhi ya watu wameamua kuondoka
katika mahema hayo kutokana na ugumu wa maisha katika eneo hilo ikiwemo
kukosa huduma muhimu kama vyoo na hospitali.
"Wengine wameenda kukaa kwa ndugu zao huku wakiendelea kujishughulisha
kwani nauli ya kutoka huku kila siku uwe na sh 3,600 hivyo wameamua
kukaa huko ikifika wiki endi ndio wanakuja kuyaangalia mahema yao,"
alisema.
Elizabeth Dominick alisema watoto walioko katika eneo hilo wanaishi
katika mazingira magumu kutokana na tatizo hilo la vyoo "mimi mwenyewe
nikibanwa nikifika chooni narudi hali ni mbaya walituahidi watatuchimbia
mashimo mengine mpaka sasa wapo kimya," alisema.
Alisema mahema hayo wakati wa jua huwa yanakuwa na joto kali hali ambayo inawafanya washindwe kukaa ndani.
Bathoromeo Joseph alisema awali kulikuwa na hema la Msalaba Mwekundu
ambalo lilikuwa likitoa huduma ya afya na kupata nafuu ya matibabu.
Alisema wanashindwa kujenga nyumba za kudumu kutokana na kipato chao
kuwa cha chini hali ambayo inawashinda hata kununua dawa kwa ajili ya
kuweka katika vyoo ambavyo kwa sasa ni hatarishi kwa maisha yao.
Alisema pamoja na kuwapatia huduma ya maji safi na umeme, bado
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni muhimu katika jamii.
Alisema akiwa kama kiongozi wa eneo hilo amewashauri wakazi hao kuanza
kuchimba mashimo ya choo ili kujinusuru na magonjwa ya milipuko ambapo
mpaka sasa bado hayajaweza kukamilika.
NIPASHE ilipowasiliana na Mkuu wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik,
alisema wakazi hao kwa sasa wanatakiwa kujitegemea badala ya kuisubiri
serikali iwafanyie kila kitu.
Alisema wajibu wa wakazi hao ni kujijengea vyoo kwani walivyojengewa kwa msaada vilikuwa ni vya muda.
Alisema serikali ina nia nzuri ya kuwasaidia lakini kwa sasa haina uwezo
huo na kuwataka kujijengea misingi ya kujisaidia wao wenyewe.
Kuhusu suala la zahanati alisema analifanyia kazi na kwamba mifuko ya
saruji iliyotolewa na wasamaria wema kama msaada itatumika kufyatulia
matofali kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.
0 Comments