SAKATA la umri wa msanii wa filamu nchini, Elizabeth
Michael maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya mauaji, sasa
limepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani,
Septemba 17, 2012.
Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu ,akituhumiwa kumuua msanii mwenzake, Steven
Kanumba. Anadaiwa kutenda kosa hilo April 7, 2012, nyumbani kwa
marehemu, Sinza jijini Dar es Salaam.
Habari zilizopatikana
kutoka mahakamani hapo na kuthibitishwa na mmoja wa mawakili wa msaniii
huyo, zinaeleza kuwa , shauri hilo litasikilizwa na jopo la majaji
watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni January Msoffe, Bernard Luanda
na Katherine Oriyo.
Mahakama ya Rufani itafanya marejeo ya
uamuzi wa Mahakama Kuu kuona kama ulikuwa ni sahihi, kukubali kufanya
uchunguzi wa umri halali wa mshtakiwa huyo, kufuatia maombi
yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka. Umri wa mshtakiwa huyo umezua
utata baada ya mawakili wanaomtetea kuomba kesi yake isikilizwe katika
Mahakama ya Watoto (Juvenile Court) wakidai kuwa bado ni mtoto.
Mawakili
hao wanaomtetea mshtakiwa huyo ni, Kennedy Fungamtama (Kiongozi wa
jopo), Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tangantyika(TLS) Peter
Kibatala na Fulgence Massawe wa Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za
Binadamu (LHRC).
Mei 7, 2012, mawakili hao waliiomba mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu iruhusu kesi hiyo isikilizwa katika Mahakama ya
Watoto wakidai kuwa, mshtakiwa huyo ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka
17 na sio 18 kama hati ya mashtaka inavyoonyesha.
Hata hivyo
Mahakama hiyo iliyakataa maombi hayo baada ya kupingwa na upande wa
mashtaka ulioongozwa na wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda ambaye
aliomba wapewe muda zaidi kwa kuwa bado upelelezi ulikuwa ukiendelea na
kwamba upelelezi huo unahusisha suala la umri.
Wakili Kaganda
aliongeza kuwa hata jina la mshtakiwa katika cheti cha kuzaliwa
kilichotajwa na mawakili wake, linasomeka kamam Diana Elizabeth wakati
mahakamani mshtakiwa anatambulika kama Elizabeth.
Katika uamuzi
wake, Hakimu Mkazi Agustina Mmbando alisema kuwa kwa kuwa kesi hiyi ni
ya mauaji na upelelezi haujakamilika, mahakama haiwezi kuamua hoja
yoyote, badala yake aliutaka upande wa utetezi kuwasilisha maombi hayo
Mahakama Kuu.
Kufuatia uamuzi huo, Mei 15, 2012 upande wa utetezi
uliwasilisha maombi Mahakama Kuu ukiomba mahakama hiyo iamuru kuwa
Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kufanya uchunguzi wa umri halali wa
mshtakiwa huyo au Mahakama Kuu yenyewe iamue kuchunguza umri wa
mshtakiwa.
Juni 11, Mahakama Kuu ilikubali maombi ya mawakili wa
mshtakiwa huyo kufanya uchunguzi wa umri sahihi wa mshtakiwa huyo, baada
ya Mahakama ya Kisutu kuyakataa. Mahakama Kuu ilitarajiwa kuanza
uchunguzi huo wa umri halali wa mshtakiwa huyo Juni 25, 2012, kwa
kusikiliza hoja za kila upande na kupitia vielelezo mbalimbali kuhusu
umri wa mshtakiwa huyo.
Hata hivyo hatua hiyo ilikwama na
kulazimika kusimama baada ya upande wa mashtaka kuitaarifu kuwa
umewasilisha Mahakama ya Rufani maombi ya marejeo ya uamuzi wa Mahakama
Kuu kukubali kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa huyo, kama ulikuwa
sahihi.
Vielelezo vilivyowasilishwa Mahakama Kuu na upande wa
mshtakiwa ambavyo ni hati za viapo vya wazazi wa mshtakiwa (mama,
Lucresia Augustin Kalugila na baba, Michael Kimemeta), cheti cha
kuzaliwa na cha ubatizo vya mshtakiwa vinaonesha kuwa ana umri wa miaka
17.
Vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16, 1995
katika kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba
B.0318479 cha Julai 23, 2004.
Lakini vielelezo ya upande wa
mashtaka navyo vinaonyesha kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa zaidi ya
miaka 18 yaani miaka 21. Vielelezo ni pamoja na maelezo ya mshtakiwa
huyo aliyoyatoa polisi wakati alipohojiwa kuhusiana na tuhuma
zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria (Passport) na maombi ya
leseni ya udereva. Pia kuna mkanda wa video aina ya CD ya mahojiano kati ya mshtakiwa huyo na mtangazaji wa kituo kimoja cha runinga nchini.
0 Comments