Mwezi mmoja tu tangu maafa ya kuzama
kwa boti ya Mv Skagit iliyotokea Chumbe Unguja Julai 18, watu wengine 10
kati ya 12 wamenusurika kufa kwenye bahari kuu kati ya Pangani, Tanga
na Mkoa wa Kaskazini Unguja baada ya boti Mv Saluwat waliyokuwa
wakisafiria kuzama.
Katika ajali hiyo iliyotokea jana, watu wawili, Khalfan Saleh Ali ambaye
ni mmoja wa mabaharia wa chombo hicho na mwingine mwanamke,
hajajulikana jina, wanahofiwa kufa maji kwa kuwa hadi jioni walikuwa
hawajapatikana.
Walionusurika ni Athumani Makame Athumani (40) wa Mtoni Kidatu, nahodha
Ali Idi Haji (51) wa Pita na Zako, Shaame Ali Shaame (33) wa Mtoni
Kidatu, Khamis Juma Mtwana (33) wa Kibeni, Ahmada Haji Kombo (47) wa
Shangani Mkokotoni, Athumani Ali Shaame (50) wa Magogoni na Fundi Khalid
(49) wa Kizimbani Pita na Zako.
Raia wa kigeni walionusurika ni Banmin Luubih (30) na Jeenle Rog (29), Raia wa Wafaransa na Ruud Verhees (23) wa Uholanzi.
Watu hao walikuwa katika boti hiyo iliyotoka bandari ya Pangani asubuhi
juzi ikienda bandari ndogo ya Mkokotoni ikiwa na abiria 12 na magunia ya
nazi.
Kati ya watu waliookolewa kutokana na jitihada za wavuvi wa bandari
ndogo ya Shangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, walikuwemo raia watatu wa
kigeni.
Fundi mkuu wa boti hiyo, Khalid Haji Maulid, alisema iliondoka Pangani
saa 2.30 asubuhi siku ya Jumapili na ikaanza kupata dhoruba na kuingiza
maji kwenye chombo majira ya saa 9 mchana.
Alisema walijitahidi kuyatoa maji kwa kutumia pampu, lakini mashine hiyo nayo ilipungua nguvu na kuharibika.
Fundi Khalid alisema waliamua kurudi bandarini Pangani, lakini
hawakufika mbali kwani chombo kilizidi kuingiza maji na injini yake
ikazimika.
“Abiria wote tuliwapa life jacket kwa ajili ya kujiokoa. Wengine
walikuwa wakielea huku wameshika chombo na waliokuwa wakijua kuogelea,
walijirusha kwenye maji,” alisema fundi huyo ambaye alikuwa mmoja wa
wafanyakazi wa boti hiyo inayomilikiwa na Ahmad Haji Kombo, mkazi wa
Shangani, Mkokotoni.
Alisema walilazimika kufanya kazi usiku kucha kuelekeza abiria
wasikumbwe na mawimbi kwa kushikilia sehemu ya juu ya chombo, lakini
hatimaye chombo kilizama kabisa usiku wa manane.
Fundi Khalid alisema akiwa na nahodha wa chombo, Ali Idi Haji, walitoa
ripoti ya tukio hilo kwa vituo vya polisi wanamaji bandarini Pangani na
Tanga mjini, lakini hawakupata msaada wowote haraka.
“Tuliwafahamisha tangu majira ya saa 9 mchana kuwa tupo eneo la Maziwe
tunahitaji msaada wa haraka, lakini bahati mbaya hadi kunakucha
hatukuwaona,” alisema.
Fundi Khalid alisema kutokana na kuchelewa kupata msaada wa polisi
wanamaji, waliwasiliana na wavuvi wanaowafahamu wanaoishi Shangani
Mkokotoni.
Hata hivyo, wavuvi hao walishindwa kutoka haraka kutokana na maji kuwa
yamejaa ambapo walisubiri hadi usiku wa manane yalipokupwa ndipo
wakaanza safari ya kuwatafuta ili kuwapa msaada.
Alisema watu wawili ambao hawajapatikana, mwanamke na mwanamume, walipotea alfajiri baada ya kuishiwa nguvu.
Chombo hicho kilisajiliwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) kwa namba Z907 SV kikiwa na uwezo wa kuchukua abiria 50.
Mvuvi aliyeongoza operesheni ya kuokoa watu hao, Rajabu Hamad Juma,
aliiambia NIPASHE kuwa alipokea taarifa majira ya saa 11 jioni juzi
kutoka kwa watu waliokuwa kwenye boti hiyo wakiomba msaada baada ya
chombo kuzidiwa na maji.
Alisema walianza safari baada ya maji kupwa usiku wa manane wakitumia
tochi na taa za kandiri kwenda eneo la tukio la Maziwe walikoelekezwa.
Ilipofika saa moja asubuhi jana ndipo walipowaona watu hao na
walifanikiwa kuwaokoa wakiwa salama na kuwapakia katika boti yao ya MV
Tawakal.
“Laiti kungekuwa na vyombo vya kisasa watu hao wangeokolewa mapema zaidi,” alisema.
Kamanda wa kikosi cha Polisi wanamaji Zanzibar, Martin Lissu alisema
walipokea taarifa za tukio mapema wakiwa kituoni kwao Malindi, lakini
kulikuwa na tatizo kubwa la mawasiliano kati yao na polisi wanamaji wa
bandari ya Tanga.
Kamanda Lissu alisema polisi wenzao wa Bandari ya Tanga waliokuwa karibu
zaidi na eneo la tukio walikuwa wamewaeleza kuwa wamechukua hatua za
kufika eneo hilo, lakini hawakuwaona watu haraka.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ZMA, Abdalla Hussein Kombo, alisema mamlaka
yake ambayo haikutoa msaada wowote kufika eneo la tukio, inakabiliwa na
tatizo kubwa la ukosefu wa vifaa vya mawasiliano na boti maalum.
Aliwasifu wavuvi wa Shangani Mkokotoni waliofanikiwa kutoa msaada na kuokoa abiria.
Baadhi ya walionusurika walipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ya Kivunge kupatiwa huduma ya kwanza.
Tukio hilo linakumbusha matukio mawili ya kuzama kwa Mv Spice Islander I
Septemba 10, 2011 na MV Skagit Julai 18 mwaka huu, ambazo ziliua mamia
ya watu na wengine kunusurika.
Ajali hii inafanya ajali kubwa za boti kufikia tatu ndani ya mwaka
mmoja tangu Septemba 10, mwaka jana ambapo watu 1,529 walikufa na 941
kuokolewa baada ya meli ya MV Spice Islanders kupinduka na kuzama
katika mkondo wa bahari eneo la Nungwi Zanzibar.
Meli hiyo ilizama kutokana na kuzidisha abiria na mizigo; kitendo
kilichopelekea viongozi kadhaa wakiwemo maofisa na vigogo wa Shirika la
Bandari na Mamlaka ya Usafiri Baharini kusimamishwa na kufunguliwa
mashitaka ya uzembe na kusababisha vifo.
Katika ajali ya Mv Skagit iliyotokea karibu na kisiwa cha Chumbe ikiwa
na abiria 248, watoto 31 na mabaharia 9, watu 146 waliokolewa wakati 139
walikufa.
0 Comments