SERIKALI imethibitisha kuwa kitendo alichokuwa akifanya babu wa
Loliondo, Mchungaji Ambilikile Masapile, cha kutoa dawa ya kutibu
magonjwa, ukiwemo Ukimwi aliyokuwa amedai kuwa ameoteshwa na Mungu ni
cha kitapeli.
Utafiti umebaini kwamba dawa hiyo ya babu wa Loliondo ni feki na kwamba haina uwezo wa kutibu Ukimwi wala kisukari.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi,
utafiti wa kulinganisha wagonjwa wa Ukimwi na kisukari waliokunywa dawa
hiyo na wale ambao hawakunywa, umebaini kwamba hakuna utofauti wa afya
ya mgonjwa.
Alisema utafiti huo unafanywa na Taasisi ya Taifa ya
Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI), ulianza Machi mwaka huu na
kwamba unahusisha wagonjwa 200 wanaofuatiliwa kwa kupimwa damu, kinga ya
mwili (CD4) na uzito wa mgonjwa, ambao ulifanyika tangu mgonjwa
alipokunywa kikombe cha babu.
“Matokeo ya awali ya utafiti
yameonyesha kuwa hakuna utofauti katika vipimo vya kimaabara pamoja na
damu, CD4, uzito na ubora wa afya ya wagonjwa kati ya waliokunywa na
wale ambao hawakunywa dawa ya mchungaji,” alisema Dk. Mwinyi.
Alisema lengo la utafiti huo ni kubaini uwezo wa dawa hiyo katika kutibu
magonjwa aliyosema dawa yake inayatibu ili kuona kama kuna utofauti
wowote baada ya mgonjwa kutumia dawa.
Kufuatia hali hiyo, jeshi la
polisi nchini limesema kwamba linafuatilia kwa makini sakata la
Mchungaji Masapile anayeishi katika kijiji cha Samunge mkoani Arusha
kufuatia malalamiko ya wananchi kuwa licha ya dawa yake kuonekana
haitibu, bado watu wanakwenda na kunywa.
Akizungumza na gazeti hili
hivi karibuni ofisini kwake makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es
Salaam, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, amesema kwamba
kutokana na malalamiko hayo polisi watawasiliana na wizara ya afya ili
kuchukua hatua stahiki.
Msemaji huyo amesema kwamba wanataka kujua
kama wizara ya afya imepiga marufuku dawa hiyo au inasema nini baada ya
kubainika kuwa haitibu na amewataka wananchi kutoenda huko.
Wananchi wengi waliozungumza na gazeti hili wamedai kwamba Babu
amewatapeli wananchi na kinachowauma ni kuona kuwa kuna watu wanaendelea
kwenda kunywa kikombe japokuwa hawatangazwi.
“Wananchi wengi
waliuza mali zao na kukimbilia kwa babu kupata tiba, kumbe ulikuwa ni
utapeli, ukweli ni kwamba serikali imechelewa mno kutoa tangazo hili,”
alisema mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja tu la John.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Vyama vya Watu Wanaoishi na Virusi vya
Ukimwi nchini (TAMOPHA), Julius Kaaya, ameitupia serikali lawama
kwa kuipigia debe dawa ya Babu na kuwafanya wagonjwa kutoroka
hospitali huku wengi wao wakiacha kuendelea na dawa wakiamini
wangepona baada ya kunywa kikombe kimoja .
“Huyu Babu inatakiwa
ashitakiwe apelekwe mahakamani afilisiwe mali zake zote alizochuma
toka kwa wagonjwa na ikiwezekana afungwe ili iwe fundisho kwa watu
wengine,” alisema Kaaya na kuongeza kuwa wao wanajiandaa kumfungulia
kesi.
Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste (TAG) Mkoani Arusha, Steve
Wambura, amemtaka babu huyo amrudie Mungu kwa kutubu kuwa aliwatapeli
wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Waganga wa Tiba Asili Mkoa wa Dar es
Saalam, Maneno Tamba, amesema babu huyo siyo mwanachama wao na
walishangazwa na serikali kumpigia debe, hali iliyosababisha vifo vya
watu wengi waliomkimbilia na kuacha tiba sahihi.
Baadhi ya mawakili,
akiwemo Mabere Marando wamesema kwamba wapo tayari kumfikisha
mahakamani babu huyo wakijitokeza waliotapeliwa na watamfungulia kesi ya
kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
0 Comments