Tokyo-Japan
LONDON, Uingereza
MIJI ya Sydney na Melbourne ni miongoni mwa maeneo yanayotajwa kuwa na gharama kubwa zaidi za maisha duniani.
Miji hiyo ambayo iko nchini Australia, imeingia katika nafasi ya tano bora.
Kwa
mujibu wa utafiti uliofanywa na Kitengo cha Kiintelijensia cha Uchumi
Duniani (EIU), gharama za maisha katika miji hiyo imezidi hata miji ya
Ulaya na Marekani.
Bara la Asia na Australia lina miji 11 kati ya 20
iliyotajwa kuwa na gharama za juu za maisha duniani, huku miji minane
ikitoka Ulaya na mmoja ukitoka America ya Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kitengo
hicho, licha ya bara la Amerika ya Kaskazini kuwa na nchi maarufu na
zenye uchumi wa juu, hakuna hata mji mmoja ulioweza kuingia kwenye 20
bora.
Katika utafiti uliofanyika miaka 10 iliyopita kulikuwako na
miji sita kutoka barani Asia, 10 kutoka Ulaya na minne kutoka Marekani
katika 20 bora kwenye orodha ya miji 131 yenye gharama za juu kwenye
nchi 93 duniani.
Katika utafiti uliotolewa mwaka huu, Jiji la
Tokyo limeshika nafasi ya kwanza likiliweka pembeni Jiji la Zurich
ambalo lilikuwa kwenye nafasi hiyo na kuporomoka hadi kufikia nafasi ya
saba.
Hii ni kutokana na sera za udhibiti wa mapato ya ndani ya nchi ya Uswiz kushuka.
Mji wa Osaka nchini Japan unashikilia nafasi ya pili katika orodha hiyo.
Jon Copestake, mhariri wa jarida la EIU alisema
moja kati ya mabadiliko yaliyojitokeza ilikuwa ni kupanda kwa gharama
nchini Australia, kulikouweka Mji wa Sydney kushika nafasi ya tatu huku
Melbourne ikishika nafasi ya tano. Mji wa Oslo wa Norway ukishika nafasi
ya nne. “Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, miji ya Australia
haikuweza kuingia hata kwenye hamsini bora. Sijawahi kuona upandaji huu
wa ghafla,” Copestake aliliambia Reuters.
“Lakini hii inatokana na kukua kwa uchumi
kunakoendana na mfumuko wa bei pamoja na kuimarika kwa Dola ya
Australia dhidi ya Dola ya Marekani. Wageni wanaofika hapo huona kuna
tofauti kubwa ya kimaisha huku wenyeji wakizoea maisha ya juu.
Kupanda kwa gharama barani Asia
Utafiti
huo ulifanyika kwa kuangalia gharama za zaidi ya bidhaa 160 ukilenga
kwenye vyakula, mavazi, huduma za nyumbani, usafiri na vitu
vidogovidogo.
Copestake haikushangaza sana kwa Mji wa Tokyo
kurejea kwenye miji ya inayoongoza, hii ni kutokana na kukua kwa uchumi
wa Japan jambo linalosababisha kuongezeka kwa gharama za mahitaji muhimu
kama vile mapango ya nyumba, mishahara na hata bei za nishati ya
mafuta.
Tangu mwaka 1992 Tokyo imekuwa kwenye sita bora huku miji ya Zurich, Paris na Oslo ikidaiwa kushika nafasi ya kwanza.
Miji mingine iliyoingia kwenye 10 bora kwa mwaka 2013 ni Singapore, Zurich, Paris,Caracas na Geneva.
Akizungumzia kuhusu nchi za Ulaya, Copestake
alisema woga wa kushuka kwa uchumi wao na kuimarika kwa Euro kumechangia
kwa kiasi kikubwa kupanda kwa gharama za maisha kwa miji ya bara hilo,
huku kwa Mji wa Carcas kumetokana na kukua kwa udhibiti wa viwango vya
ubadilishaji wa fedha.
Licha ya kutokuwako kwa miji ya Amerika ya Kaskazini kwenye 20
bora, EIU imesema gharama za maisha kwa mji wa Washington zilikuwa
zikiongezeka ukilinganisha na maeneo mengine ya Marekani. Mji huo
umeshika nafasi ya 27 ukifungana na Mji wa Los Angeles.
Mji wa
Vancouver wa nchini Canada umeendelea kushika nafasi ya 21, ukiwa ni mji
wenye gharama za juu zaidi za maisha kwa nchi za Amerika ya Kaskazini.
Hata hivyo, wakati Bara la Asia na Australia kuna
jumla ya miji 11 iliyoingia kwenye 20 bora, inasemekana ni eneo ambalo
lina miji sita kati ya 10 yenye gharama rahisi zaidi duniani.
Mji wa
Mumbai kutoka nchini India na Karachi wa Pakistan ni miongoni mwa miji
iliyotajwa kuwa na gharama za chini za maisha katika utafiti huo
ikifuatiwa na New Delhi, Kathmandu na Algiers.
Nchi ya India imekuwa na tofauti kubwa kimaisha kwa baadhi ya miji kutokana na kuwepo kwa tofauti ya mgawanyo wa miundombinu.
Hii ndiyo sababu kubwa ya kuweko kwa miji yenye gharama za juu zaidi na ile yenye gharama za chini zaidi.
Miji mingine iliyoshika nafasi kumi za mwisho
katika utafiti huo ni pamoja na Bucharest wa Romania, Colombo wa Sri
Lanka, Panama City, Jeddah wa Saudi Arabia, na Teheran wa Iran.
Imetafsiriwa na Maimuna Kubegeya kwa msaada wa mtandao
0 Comments