Maharusi.
UTAFITI mpya wa masuala ya uhusiano umebainisha kuwa watu wenye
umri kati ya miaka 35 na 40, ambao hawajaoa au kuolewa wapo kwenye
hatari ya kufa mapema tofauti na waliooa au kuolewa.
Matokeo ya utafiti huo, uliofanywa hivi karibuni
na wataalamu wa masuala ya uhusiano ukiongozwa Dk Ilene Siegler wa Idara
ya Sayansi ya Tabia kutoka Chuo Kikuu kilichopo Kaskazini mwa Jimbo la
Carolina nchini Marekani, umebainisha pia kwamba ndoa ni kinga
inayomwongezea binadamu muda wa kuishi.
Aidha, watafiti hao wamebainisha kwamba wanawake
waliopewa talaka au kufiwa na wenza katika umri wa kati wapo kwenye
hatari ya kufa mapema zaidi.
Watafiti hao wameeleza kuwa watu ambao maishani
hawajawahi kuoa au kuolewa wapo kwenye hatari ya kufa mapema mara tatu
zaidi ya wale waliokuwa katika ndoa imara katika maisha yao, hasa
wakiwa kwenye umri wa kati.
Matokeo hayo ambayo yalichapishwa kwenye jarida
la Annals journal la Marekani na kuandikwa kwenye mtandao wa Daily
Mail, ulihusisha watu 4,802, wakiwamo watu waliozaliwa miaka 40
iliyopita.
Ulibaini kuwa kati ya watu wazima wenye umri kama huo wengi wao walikufa wakiwa na miaka 50, kutokana na kuishi peke yao.
Kwa kutumia dodoso na maswali ya moja kwa moja
walibaini kuwa pamoja na mtu aliyekuwa kwenye ndoa kuishi kwenye maisha
hatarishi kwa kunywa pombe kupita kiasi na kuvuta sigara, bado walio
kwenye ndoa wana nafasi ya kuishi muda mrefu zaidi kwa asilimia 2.3.
Dk Ilene Siegler, anasema kuwa maisha ya kwenye ndoa ni kinga inayowafanya wanandoa waishi kwa muda mrefu.
“Inaonyesha kuwa na mke au mume ni kinga ya maisha
hasa katika umri wa kati, hali hii ikiwaathiri zaidi wanaume, kuliko
wanawake,”amesema Siegler.
Alisema kuwa utafiti huo umewawezesha kubaini kuwa
kati ya vifo 238 vilivyotokana na athari za kutokuoa au kuolewa,
wanaume ndiyo waliothirika zaidi na kwamba kati yao wanawake walikuwa ni
32 tu.
Alifafanua kuwa wanaume wameathirika zaidi
kutokana na kutokuwa karibu na familia, hivyo kufanya mambo tofauti na
mwanamke, ambao hata kama hajaolewa anaweza kuwa karibu na familia na
kupata ushauri wa baadhi ya mambo, ingawa hali hiyo haimfanyi kuwa
salama,”anasema Siegler.
Dk Siegler alitolea mfano utafiti uliofanywa hivi
karibuni na nchi saba za Ulaya akieleza kwamba utafiti huo umeonyesha
kuwa mtu aliye kwenye ndoa huwa na furaha kimwili, kiakili na kiafya na
humfanya awe na marafiki wazuri, pia hupata ulinzi kwa kuwa wanandoa
wana kawaida ya kujilinda wenyewe.
0 Comments