Serikali ya Malawi imekubali kurudi katika meza ya mazungumzo kuhusu mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa kati yake na Tanzania.
Malawi imechukua uamuzi huo baada ya hivi karibuni Rais wa nchi hiyo, Joyce Banda, kutangaza kujiondoa katika mazungumzo hayo.
Hatua ya kuendelea kwa mazungumzo hayo ilitangazwa jana na Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule, wakati
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Haule alieleza uamuzi huo baada ya waandishi wa habari waliohudhuria
uzinduzi wa Wiki ya Umoja wa Mataifa kumuuliza kuhusu hatma ya mgogoro
huo kati ya nchi hizo mbili baada ya Malawi kujiondoa katika mazungumzo
na kutaka kulipeleka suala hilo katika Mahakama ya kimataifa ya
Uusuluhishi wa Migogoro (ICJ).
Akijibu alisema: “Kuhusu swali ulilouliza, wenzetu wa Malawi watakuja nchini kuanzia tarehe 27, Oktoba.”
Alisema baada ya ujumbe wa Malawi kuwasili nchini, vikao vya mazungumzo kuhusu mgogoro huo wa mpaka wa Ziwa Nyasa vitaanza.
Hata hivyo, Haule hakulitolea ufafanuzi zaidi suala la mazungumzo ya
kusaka amani katika mzozo wa mpaka huo ambao katika miezi ya karibuni,
ulisababisha kuzorota kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili, ambazo ni
wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
Mwezi uliopita, Rais wa Malawi, Joyce Banda, muda mfupi baada ya
kuwasili nchini humo akitokea New York, Marekani alikokutana na kufanya
mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alitangaza
nchi yake kujitoa katika meza ya mazungumzo kuhusu mgogoro huo wa mpaka
katika Ziwa Nyasa na kutangaza kuupeleka ICJ.
Kwa mujibu wa Banda, serikali yake iliamua kuchukua hatua hiyo kwa madai
kuwa Tanzania imevuruga makubaliano yaliyofikiwa nchini humo ya
kuendelea katika meza ya mazungumzo baada ya kuchora ramani mpya
inayoonyesha kuwa mpaka unapita katikati ya Ziwa Nyasa, kuweka bendera
katika eneo lenye mzozo na wavuvi wa Malawi kunyanyaswa.
Kabla ya kwenda New York, Rais Banda, alikutana na Rais Jakaya Kikwete,
mjini Maputo Agosti 17, mwaka huu na kufanya mazungumzo, ambayo
yalimridhisha Rais Banda kwamba mgogoro huo wa mpaka hauwezi kusababisha
vita kati ya Tanzania na Malawi.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi
na serikali wa Sadc, Rais Kikwete alisema kuwa Tanzania haina mpango
wowote wa kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Malawi.
Alisema kuwa yeye akiwa Amiri Jeshi Mkuu, hajawahi kuwa na wazo la
kutumia nguvu za kijeshi katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa
Tanzania, Bernard Membe, alisema mahakama hiyo isingeweza kusuluhisha
mgogoro huo kwa kuwa Tanzania haijasaini mkataba wa kuanzishwa kwake.
Rais Kikwete alipokutana na Ban Ki-moon mjini New York mwezi uliopita,
alipongezwa kwa kutumia mazungumzo katika kumaliza mgogoro wa Ziwa
Nyasa.
Mgogoro huo unatokana na Tanzania kusema kuwa kila nchi inamiliki mpaka
wa Ziwa Nyasa kwa asilimia 50 wakati Malawi ikisema inalimiliki kwa
asilimia 100.
Mazungumzo ya awali, yaliwashirikisha mawaziri na wataalam kabla ya Malawi kujitoa yalifanyika Dar es Salaam na Muzuzu.
0 Comments