Dk Slaa
SASA ni dhahiri sumu aliyoimwaga Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa na makada wengine wa chama hicho mjini Moshi wiki
iliyopita, imeanza kukitafuna Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jimbo la Moshi Mjini, limekuwa likishikiliwa na
kambi ya upinzani tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995,
huku Chadema kikiigaragaza CCM katika kiti cha ubunge mara tatu
mfululizo.
Makada wa CCM wamejitokeza na kuhoji ukimya huo wa
CCM wakati sumu hiyo imeanza kusambaa kwa kasi miongoni mwa wananchi na
kukiweka chama hicho njiapanda uchaguzi mkuu 2015.
Kada wa CCM, Ramadhan Mwindad ‘Gadaffi’ jana
alizua kizaazaa katika ofisi za CCM Moshi Mjini, alipoamua kujitoa
mhanga na kwenda kuwahoji viongozi sababu za kutojibu mapigo. Tukio hilo
lililovuta hisia za watu wengi, lilisababisha kada huyo na kiongozi
mmoja wa CCM ngazi ya wilaya kushindwa kujibu hoja na kudai kada huyo
ametumwa na Chadema.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea
mbele ya Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Paul
Matemu na Katibu Mwenezi wa Mkoa huo ambaye pia ni Diwani, Michael
Mwita.
“Mimi ni kada wa CCM nimekwenda pale saa 8:00
mchana huu (jana) na kuwauliza kwa nini kila siku mnafanya vikao vya
ndani vya kikatiba, lakini hamwendi kwa wananchi kujibu mapigo?”alisema.
Badala yake, kada huyo alisema kiongozi huyo ngazi
ya wilaya alimjia juu na kumtuhumu kuwa ametumwa na Chadema kuhoji
mambo hayo na kukwepa kabisa kujibu hoja ya msingi.
“Viongozi wa kitaifa wametukanwa na kudhalilishwa
sana.Mkuu wetu wa mkoa mpaka imefikia mahali ameitwa ki model
(mwanamitindo) bado viongozi wetu wamekaa kimya,”alisema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na kada mwingine wa CCM
Kata ya Longuo, ambaye alisema baadhi ya viongozi walijinadi kwa
mbwembwe katika uchaguzi uliopita lakini sasa wanachama hawaoni makeke
yao.
“Kuna viongozi walijinadi kwa wapiga kura kuwa
oooh hili ni jembe mchagueni, mbona kimya? Hata kujibu tu matusi na
kejeli za mkutano ule wa Chadema wameshindwa”alisema kada huyo.
Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini, Elizabeth Minde alipoulizwa jana kuhusu
madai ya wanachama wake alisema yuko kwenye kikao na pindi atakapomaliza
tu angelipigia gazeti hili kutoa ufafanuzi.
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Mwita
alipoulizwa kuhusu tafrani hiyo alisema hakuona kama kulikuwa na
mabishano katika ofisi hizo za CCM kwa kuwa alikuwa mbali kidogo na eneo
la tukio.
“Nilimwona Gadaffi na (jina la kiongozi wa wilaya)
wakizungumza ila sikujua wanazungumzia nini, lakini nataka ifahamike
CCM ina utaratibu wake wa kuitisha mikutano na hatujibu matusi,”
alisema.
0 Comments