ASEMA MATUMIZI YA SILAHA ZA MOTO HAYATATUI MIGOGORO, ASKARI WALIOKAMATWA IRINGA, KUFIKISHWA KORTINI JUMATATU
Lilian Lucas, Morogoro
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye
amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuacha kutumia silaha za moto au nguvu
ya ziada linapokabiliana na raia, badala yake litumie busara kutatua
migogoro.Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, baada ya
kufunga mafunzo wa wahariri wa vyombo vya habari yaliyohusu utawala,
Sumaye alisema kufa mtu katika mapambano ya polisi na raia siyo kitu
kidogo.
Kauli hiyo ya Sumaye inaonekana kuwalenga polisi ambao
wanadaiwa kusababisha kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa
Televisheni ya Channel Ten mkoani Iringa, David Mwangosi.
Mwandishi
huyo aliuawa Jumapili iliyopita katika Kijiji cha Nyololo, Iringa kwa
kulipuliwa na kitu kinachodhaniwa kuwa bomu, wakati polisi walipokuwa
wakiwazuia viongozi na wanachama wa Chadema kukusanyika wakati
wakifungua tawi la chama hicho kijijini hapo.
Mpaka sasa askari
watano wa jeshi hilo, akiwamo anayetuhumiwa kumlipua kwa bomu marehemu
Mwangosi, wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa na jeshi hilo mkoani
Iringa.
Sumaye alisema kuwa katika siku za karibuni, polisi
wamekuwa wakikimbizana na raia mara kwa mara pamoja na kutumia silaha na
nguvu isiyo ya kawaida hata pale pasipostahili. Jambo ambalo alisema
siyo sahihi kwa mustakabali wa jeshi hilo.
“Si lazima sana kwa
polisi kutumia silaha hasa za moto kila wakati. Nimekuwa nikitazama
kwenye televisheni mara kwa mara na kuona polisi wakitumia silaha, hata
sehemu za kuvunja nyumba tu huko vijijini. Nawashauri watumie busara,”
alisema Sumaye na kuongeza:
“Tusidhani risasi inaweza kutatua
migogoro wakati wote. Risasi inaweza kuharibu kila kitu, zitumike pale
inapokuwa ni lazima kwani Watanzania siku zote si watu wa fujo.”
Alisema
kutokana na tukio la hivi karibuni la kuuawa kwa mwandishi wa habari,
Serikali, Polisi na vyombo vingine vya usalama, watakuwa wamejifunza
kitu katika kutatua migogoro na migongano baina yao na wananchi
wanaowaongoza.
Alisema kwamba Jeshi la Polisi nchini linapaswa
kutambua kuwa matumizi ya nguvu kupita kiasi ikiwa ni pamoja na kutumia
risasi kutawanya raia, si suluhisho la migogoro baina yake na wananchi,
bali kinachohitajika ni busara zaidi, ili kuepusha maafa.
Akizungumzia
suala la polisi kupambana na wanasiasa alisema, mazingira ya siasa kwa
sasa yamechangamka zaidi ikilinganishwa na yale ya zamani na kwamba
wakati mwingine wanasiasa wamekuwa wakichangia vurugu na hivyo
kulilazimisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu ya ziada.
“Sisi
wanasiasa tusiwe kichocheo cha kuleta vurugu na badala yake tutumie njia
za kistaarabu na si kuchokoza vyombo vya usalama. Kinachotakiwa busara
zitumike pande zote, vinginevyo tutaendelea kuumiza watu,” alisema.
Kuhusu
uhusiano baina ya Serikali na waandishi wa habari, Sumaye alisema
kinachoathiri hali hiyo katika nchi za Afrika ni kutokana na baadhi ya
Serikali kutotaka mambo yake yawe wazi. Alisema katika mazingira mengi
hata pale unapokuwapo uhusiano huo unakuwa wa kinafiki usioleta tija kwa
pande zote.
Alisema iwe ni polisi na wananchi au polisi na
waandishi, busara zitumike zaidi badala ya nguvu katika kutafuta
suluhisho kwani siku zote mapambano hayatatui na badala yake, yanaweza
kuharibu kabisa amani iliyopo.
Akifunga mafunzo hayo ya siku nne
yaliyohusu utawala, Sumaye alisema vyombo vya habari ni sehemu ya maisha
ya kila siku katika jamii kwa kuwa vina habarisha mambo muhimu kwa
maendeleo ya taifa.
Alisema vinatoa taarifa ya nini Serikali
zinawafanyia watu wake na nini hazifanyi ili wananchi waweze kudai haki
zao na hata kuikumbusha wajibu wake pale inapojisahau. Muda mwingine
vyombo vya habari vimekuwa kisu kikali kwa sababu si Serikali zote
zinazopenda kukosolewa, kukumbushwa na kupewa changamoto kwa yale
zilizoyafanya na zinayopaswa kuwafanyia wananchi wake.
“Vyombo vya
habari ni kama kioo tunachojitazama kila asubuhi kabla kutoka nyumbani
kwenda ofisini au kuhudhuria mikutano muhimu, ili kujua kama umevaa
uhusika wa kile unachokwenda kukifanya au kukizungumza mbele ya jamii.
Huwezi kuvunja kioo kama kitakuonyesha kitu ambacho huhitaji kukiona
kwenye mwonekano wako.
Hivyo si sahihi kuvilaumu au kuviadhibu vyombo vya habari pale vinapokosoa na badala yake ni kujirekebisha,” alisema Sumaye.
Watuhumiwa wa mauaji ya Iringa Katika
hatua nyingine askari watano wanaoshikiliwa Iringa wanaendelea
kuhojiwa, huku taarifa zikieleza kuwa wanaweza kufikishwa mahakamani
Jumatatu, kutokana na kushindikana jana.
Jana, taarifa zilisambaa
kwamba askari hao walikuwa wafikishwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Iringa, lakini hadi jioni, walikuwa hawajafikishwa. Pia hakukuwa na
taarifa zozote za nini kilikuwa kinaendelea.
“Ni kweli walitakiwa
wafikishwe leo, lakini hadi sasa hawajafika, wakifika nitawaeleza,”
alisema mmoja wa wafanyakazi wa mahakama hiyo jana.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda hakutaka kueleza lini
watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa kile alichosema kwamba kwa
sasa yeye siyo msemaji wa jambo hilo.
“Hapa alikuja IGP (Said
Mwema), na sasa yuko DCI (Robert Manumba). Kwa mazingira haya uhuru
wangu wa kuzungumza uko limited, (una kikomo),” alisema.
Alipoulizwa
watuhumiwa hao wako mahabusu ipi, alihoji... “Wapi?” Aliendelea kusema,
“Nashindwa kusema wapo au hawapo kwa kuwa mimi siyo msemaji wa jambo
hilo, ila nawashauri m-cross-check (kuthibitisha), vizuri vyanzo vyenu
vya habari.”
0 Comments