WATU 48 WAMEUAWA MAPIGANO YA KIKABILA KENYA
Polisi
nchini Kenya, wanasema kuwa watu 48, waliuawa siku ya Jumanne usiku wa
kuamkia leo, Jumatano, kufuatia mapigano makali kati ya jamii za
Pokomo na Orma katika eneo la Mto Tana Kusini Mashariki mwa Kenya.
Mauaji
hayo yilitokea wakati watu wenye silaha kutoka jamii ya Pokomo
waliposhambulia kijiji kimoja katika eneo la Reketa huku wakiteketeza
makaazi ya watu.
Naibu kamanda wa polisi mjini Mombasa,
Joseph Kitur, amethibitisha kuwa watu 48 waliuawa, 31 kati yao ni
wanawake, watoto 11 na wanaume sita.
Ng'ombe wapatao 60 vile vile walikatakatwa na wavamizi hao.
Kitur amesema shambulio hilo ni la
kushangaza kwa kuwa watu 34 waliuawa kwa kukatakatwa mapanga, wengine
14 nao waliteketea hadi kufa katika nyumba zao.
Amesema uchunguzi wa awali umebainisha kuwa shambulio hilo lilifanywa na watu kutoka jamii ya Pokomo.
Tangu mwezi uliopita, jamii hizo mbili
zimekuwa zikipigana kuhusu umiliki wa ardhi inayotumiwa kama eneo la
malisho ya mifugo, lakini shambulio hilo la Jumatano ndilo baya zaidi
kuwahi kutokea katika historia yao.
Ripoti zinasema polisi wanawasaka wale waliofanya mashambulio hayo.
Kuna taarifa kuwa watu kadhaa wamekamatwa na polisi lakini mkuu huyo wa polisi hakuthibitisha ripoti hizo.
Idara ya polisi imesema uhasama kati ya
jamii hizo mbili umekuwa ukitokota kwa muda, lakini hapakuwa na ishara
ya fununu yoyote kuwa shambulio hilo la Jumatano lingetokea.
Mwaka wa 2001, takriban watu 130, waliuawa kwenye mapigano katika maeneo ya mipakani kati ya jamii hizo mbili.
Mbunge wa Eneo hilo, Danson Mungatana,
amesema shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi mashambulio mengine
yaliyofanywa na jamii ya Orma ambapo mamia ya mifugo iliibwa.
0 Comments